LONDON, England
Bondia Anthony Joshua amesema anataka kutumia nguvu na kimo chake ili kumtwanga mpinzani wake, Oleksandr Usyk wakati mabondia hao watakapopanda ulingoni Agosti 20 mwaka huu pambano litakalofanyika Saudi Arabia.
Joshua mwenye umri wa miaka 32 sasa, akiwa na rekodi ya kucheza mapambano 24 na kushindwa mawili huku 22 akishinda kwa KO atakuwa akiwania kutetea mikanda ya WBA, IBF na WBO katika uzito wa juu dhidi ya Usyk ambaye amepigana mara 19, hajapoteza na ameshinda kwa KO mara 13.
Tangu mabondia hao wapande ulingoni Septemba mwaka jana kwenye Uwanja wa Tottenham Hotspur na Usyk kupewa ushindi uliotolewa na majaji wote, hakuna kati yao aliyepigana hali ambayo inalifanya pambano hilo kusubiriwa kwa hamu na mashabiki wa ngumi duniani.
Pamoja na kupata ushindi katika pambano hilo, Usyk alitoka ulingoni akiwa ameumia vibaya kwenye jicho lake la kulia, tukio ambalo Joshua alilizungumzia katika namna ya dhihaka kwenye mkutano na waandishi wa habari.
“Staili yake ya nywele iko tofauti na ana kovu kwenye jicho, nikifikiria hali ilivyokuwa nimewahi kuwachana watu wachache usoni kina, Paul Butlin, Usyk na wengine, napenda mambo hayo, nayakumbuka sasa na najiandaa kuyarudia,” alisema Joshua na kuongeza kuwa wakati akipigana na Usyk aliamini kwamba alikuwa akimpiga.
“Naapa nilijua nashinda pambano nilijiona niko vizuri, nilijiona niko kama Muhammad Ali lakini ni kama vile hakukuwa na mawasiliano ya kujua nilifikia wapi ghafla ikawa kama naambiwa unashindwa, uko nyuma kwa raundi mbili, sikuelewa hilo ilikuwa ngumu kukubali,” alisema Joshua.
“Simlaumu mtu na sasa hivi nikiangalia ilivyokuwa nafikiri alishinda katika raundi tatu pengine ni kuanzia raundi ya tisa kwenda mbele.”
Ngumi Joshua apania kumtwanga Usyk
Joshua apania kumtwanga Usyk
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
