Manchester, England
Kocha wa Man United, Erik ten Hag amemtetea kiungo wake, Casemiro kwa namna alivyomlinda Antony katika mechi na Crystal Palace tukio lililosababisha kiungo huyo apewe kadi nyekundu.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye dimba la Old Trafford na Man United kutoka na ushindi wa mabao 2-1, Ten Hag pia alisema kwamba Jordan Ayew naye alipaswa kupewa kadi nyekundu.
Casemiro sasa atakosa mechi tatu za Man United baada ya VAR kumuonyesha akimkaba shingoni, Will Hughes baada ya kutokea tafrani baina ya wachezaji wa timu hizo mbili.
Katika tafrani hiyo, Jeff Schlupp ‘alimsukuma’ Antony nje ya uwanja hadi akaangukia kwenye mabango wa matangazo wakati Ayew naye alionekana akimkabili Fred.
“Unajua hawa watu kila mmoja yupo kwa ajili ya mwenzake, ni jambo zuri kwenye timu na hawapendi kuona mmoja wa wachezaji anaumizwa vibaya na hivyo ndivyo alivyofanyiwa Antony, hii timu ipo pamoja ingawa ni muhimu kuzuia hasira,” alisema Ten Hag.
“Ni jambo gumu katika tukio kama lile, unaona timu mbili wachezaji wakipigana na unaona ‘wanavuka mpaka’ lakini mchezaji mmoja tu anaangaliwa na anapewa kadi nyekundu, si sahihi,” alisema Ten Hag.
“Mchezaji wa Crystal Palace alifanya kitu hatari kwa kumchezea rafu Antony na bahati hakuumia kwa jinsi alivyomsukuma hadi akavuka mstari na baada ya hapo kila mmoja anajibu mapigo, wote wachezaji wa Crystal Palace na Manchester United,” alisema.
Ten Hag alikiri kwamba Casemiro alivuka mpaka katika kumkabili Hughes lakini picha ya video pia ilionyesha jinsi Ayew alivyomkaba Fred shingoni ingawa hakuna hatua iliyochukuliwa kwa mshambuliaji huyo wa Palace.
“Ni mchezaji ambaye alifanya kitu kibaya kuliko hata Casemiro, naye alivuka mpaka,” aliongeza Ten Hag huku akisisitiza kwamba anadhani Ayew alipaswa kupewa kadi nyekundu.
“Casemiro alikuwa anamlinda mchezaji wetu na pia alikuwa akimlinda mchezaji ambaye alitaka kupigana, alikuwa akimzuia hakutaka mchezaji aumizwe, Casemiro ndio alivuka mpaka lakini wachezaji wengine wengi nao walifanya hivyo hivyo,” alisisitiza Ten Hag.
