Paris, Ufaransa
Kocha wa PSG, Luis Enrique amemtaka mshambuliaji wake Kylian Mbappé kufanya kazi ya ulinzi katika mechi ya nusu fainali ya pili dhidi ya Borussia Dortmund leo Jumanne ili kubadili matokeo baada ya kulala kwa bao 1-0 katika mechi ya kwanza.
Enrique alikuwa akijibu swali aliloulizwa kuhusu nini anachoweza kufanya Mbappe ili kuipatia timu hiyo ushindi ambapo kocha huyo alisema mshambuliaji huyo nyota anahitaji kutoa mchango wake katika eneo lote la uwanja.
“Sisi ni timu, tunawataka washambuliaji kusaidia kuhakikisha mipira inafika mara chache kwenye eneo letu la ulinzi, kwa pamoja kila mmoja ana wajibu wa kutoa mchango wake, hata mchezaji nyota duniani anatakiwa kusaidia katika ulinzi,” alisema Enrique.
Enrique hata hivyo alisema kwamba ana matumaini ya timu yake kutoka na ushindi katika mechi hiyo na hatimaye kucheza fainali ya michuano hiyo mikubwa ya ngazi ya klabu barani Ulaya.
Kocha huyo pia alisema kwamba kitendo cha kuwa nyuma katika mechi ya kwanza si jambo ambalo linamfanya aogope badala yake anaamini timu yake ipo vizuri kimtazamo na kifikra kwa ajili ya mechi hiyo.
“Nafikiri unahitaji utulivu wa kifikra ili kukabiliana na jambo lolote katika taaluma yako au maisha yako binafsi, wakati wote jiandae mambo yanaweza kwenda vibaya kama ni lazima iwe hivyo na uwe tayari kubadili hali hiyo,” alisema Enrique.
Kwa upande wake kocha wa Dortmund, Edin Terzic alisema timu yake inahitaji kuboresha kiwango ilichokionesha katika mechi ya kwanza ili iweze kufuzu na hatimaye kusonga mbele na kucheza mechi ya fainali.