London, England
Klabu ya Chelsea hatimaye imefikia makubaliano na kocha wa zamani wa klabu za Tottenham Hotspur na PSG, Mauricio Pochettino ambaye sasa atakuwa kocha mkuu mpya wa timu hiyo.
Pochettino (pichani) hivi karibuni amekuwa akitajwa kupewa jukumu la kuinoa Chelsea ambayo inanolewa na kocha wa muda Frank Lampard aliyekabidhiwa mikoba baada ya Graham Potter kutimuliwa.
Kocha Pochettino ambaye amekuwa bila ya kazi tangu majira ya kiangazi mwaka jana alipotimuliwa PSG, na nafasi yake kukabidhiwa Christophe Galtier, ataanza kazi rasmi mara baada ya msimu huu.
Pochettino mwenye umri wa miaka 51 ambaye pia amewahi kuinoa Southampton, anakuwa kocha wa sita wa Chelsea katika kipindi cha miaka mitano.
Chelsea imekuwa na msimu mbaya ikitolewa na Man City katika Kombe la FA na lile la Ligi na hivi karibuni imetolewa na Real Madrid katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kibaya zaidi ni kwamba kwa sasa inashika nafasi ya 11 kwenye Ligi Kuu England (EPL) ikiwa na rekodi ya kushinda mechi moja tu kati ya 11 zilizopita ikipoteza mechi nane na tayari imepoteza matumaini ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Machi mwaka huu baada ya Spurs kuachana na kocha Antonio Conte, Pochettino alikuwa akitajwa kurudi katika timu hiyo akikumbukwa kuiwezesha kufikia hatua ya fainali ya Kombe la Ligi mwaka 2015 na kuiwezesha kushika nafasi ya pili kwenye EPL msimu wa 2016-17.
Kimataifa Pochettino kocha mpya Chelsea
Pochettino kocha mpya Chelsea
Read also