Nice, Ufaransa
Beki wa timu ya taifa ya Algeria anayeichezea Nice ya Ufaransa, Youcef Atal (pichani) amesimamishwa miezi minane na mahakama kwa kosa la kuweka kwenye mitandao ya kijamii video yenye kuchochea chuki za kidini.
Atal anadaiwa kutoa taarifa kupitia video hiyo, taarifa ambazo zinahamasisha chuki za kidini kuhusu mgogoro unaoendelea wa Israel na Gaza.
Mahakama hiyo ya Jinai ya Nice nchini Ufaransa sambamba na adhabu hiyo itakayomuweka mchezaji huyo nje ya soka, pia imemtaka alipe faini ya Pauni 38,800 kwa kuweka video hiyo kwenye akaunti yake ya Instagram.
Klabu ya Nice nayo imetangaza kumsimamisha hadi itakapotoa taarifa nyingine kuhusu mchezaji huyo ambaye pia jina lake limo kwenye kikosi cha Algeria kinachojiandaa kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) nchini Ivory Coast baadaye mwezi huu.
Adhabu ya mahakama pia imemtaka Atal, 27, kulipia gharama za machapisho ya kesi inayomkabili katika gazeti moja la serikali na machapisho mengineyo.
Atal hata hivyo baadaye alifuta video hiyo na kuomba radhi kabla ya kurudi kuomba radhi kwa mara ya pili akiwa mahakamani akidai awali alitaka kutuma ujumbe wa amani katika video hiyo ya sekunde 35 lakini hakuiangalia wakati anatuma.
Hoja hiyo ya Atal hata hivyo hazikuweza kuwashawishi waendesha mashtaka ili kumpunguzia adhabu au kumsamehe kwa madai kwamba hakukuwa na ujumbe wowote wa amani kwenye video hiyo.
Kimataifa Beki wa Algeria asimamishwa miezi minane
Beki wa Algeria asimamishwa miezi minane
Related posts
Read also