Na mwandishi wetu
Rais wa heshima wa klabu ya Simba, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji ameahidi kutoa fungu la kutosha kwa ajili ya kufanya usajili utakaoirudisha timu hiyo kwenye ushindani wa mataji ya ndani na nje ya nchi.
Tajiri huyo juzi aliwapongeza watani zao Yanga, kwa kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika lakini mafanikio hayo yamemfanya kuingilia kati suala la usajili wa timu yake kuelekea msimu ujao lengo likiwa ni kupata wachezaji wenye ubora unaoendana na malengo ya Simba.
Dewji ameeleza kuwa anafanya hivyo kwa kuwa hataki kuona makosa waliyofanya huko nyuma yakijirudia na hiyo inatokana na malengo waliyokuwa nayo ya kuwa miongoni mwa timu zinazopigania mataji na siyo kusindikiza wenzao.
“Natarajia kukutana na benchi la ufundi pamoja na mtendaji mkuu wa timu ili kujadili ninachotaka lazima tufanye maamuzi magumu ya kuachana na watu ambao hawana msaada kwenye timu na kuleta wachezaji ambao wataipigania timu na kutufikisha pale tunapopakusudia,” alisema Dewji.
Kiongozi huyo ameeleza kuwa zoezi hilo halitofanywa kwa wachezaji pekee bali watalifanya hata kwa baadhi ya viongozi ambao wataonekana hawana msaada ndani ya timu siyo mbaya wakawaweka pembeni ili kubaki na watu sahihi watakaoisaidia timu kufika wanapopataka.
Alisema mafanikio waliyokuwa nayo watani zao Yanga, yametokana na maamuzi magumu yaliyofanywa na uongozi ulioingia madarakani hivi karibuni hivyo hata wao kama wanataka kufanikiwa lazima wabadilike bila kumwonea huruma mtu yeyote.
Kwa mujibu wa ripoti ya Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’, timu hiyo inatarajia kusajili wachezaji wapya wanane, wengi wao wakiwa wa kigeni ili kuboresha kikosi chao na kufanya vizuri pia kwenye michuano ya klabu Afrika mwakani.