London, England
Bingwa mtetezi wa Kombe la FA, Livepool leo Jumapili imeliachia rasmi taji hilo baada ya kukubali kipipo cha mabao 2-1 mbele ya Brighton, matokeo yanayozidi kumuweka katika wakati mgumu kocha Jurgen Klopp.
Aliyechangia kuitoa Liverpool katika raundi ya nne ya mashindano hayo na kuiondoa katika mbio za kulitetea taji hilo ni winga Mjapani wa Brighton, Mitoma ambaye alifunga bao la ushindi kwa timu yake katika dakika mbili za nyongeza.
Liverpool ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao katika mchezo huo mfungaji akiwa ni Harvey Elliott dakika ya 30 akiitumia vizuri pasi ya Mohamed Salah. Dakika tisa baadaye, Brighton walisawazisha bao hilo kupitia kwa Tariq Lamptey.
Kipigo hicho kinakuwa ni mwendelezo wa matokeo mabaya kwa Liverpool dhidi ya Brighton baada ya kuchapwa mabao 3-0 na timu hiyo katika Kombe la FA wiki mbili zilizopita.
Kwa matokeo hayo Liverpool sasa inakuwa imepoteza nafasi ya kubeba taji hilo huku ikiwa na wakati mgumu katika Ligi Kuu England (EPL) na haitoshangaza ikishindwa kuwa kati ya timu nne bora za ligi hiyo ‘top four’ msimu huu.
Katika EPL, Liverpool inashika nafasi ya tisa ikiwa imeachwa katika top four kwa tofauti ya pointi 10, mwenendo ambao si mzuri kwa timu yenye hadhi ya Liverpool ambayo msimu uliopita ilifikia hatua ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kushika nafasi ya pili EPL.
Klopp amewahi kunukuliwa akisema kwamba hatoondoka Liverpool labda akilazimishwa kufanya hivyo ingawa alikiri kwamba siku zijazo upo uwezekano wa kufanyika mabadiliko katika timu hiyo.
Akijibu shutuma mbalimbali zilizoelekezwa kwake kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo, Klopp (pichani) amenukuliwa akisema kwamba hajawa kocha mbaya kwa ghafla namna hiyo.
“Sijawa kocha mbaya kwa ghafla na sijawahi kuwa kocha mzuri kama ambavyo watu wanaweza kusema na si mbaya kama ambavyo pengine watu wanaweza kufikiri,” alisema Klopp.
Aprili mwaka jana, Klopp aliongeza mkataba na Liverpool ambao sasa unafikia ukomo mwaka 2026 na kama atafikisha hadi wakati huo ataweka rekodi ya kuinoa timu hiyo kwa miaka 11 baada ya kutua mara ya kwanza Oktoba, 2015.
Akiwa na Liverpool hadi sasa ameiwezesha kubeba mataji kadhaa likiwamo la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2019 na lile la EPL mwaka 2021 na ingawa anakiri msimu huu ni mgumu lakini bado ana matumaini.
Matokeo ya mechi za Jumapili Kombe la FA…
Brighton 2-1 Liverpool
Stoke 3-1 Stevenage
Wrexham 3-3 Sheff Utd
Matokeo ya mechi za Jumamosi Kombe la FA…
Accrington 1-3 Leeds United
Walsall 0-1 Leicester City
Blackburn 2-2 Birmingham City
Bristol City 3-0 West Bromwich
Fulham 1-1 Sunderland
Ipswich Town 0-0 Burnley
Luton Town 2-2 Grimsby Town
Sheffield Wednesday 1-1 Fleetwood Town
Southampton 2-1 Blackpool
Preston North 0-3 Tottenham
Man United 3-1 Reading