Na mwandishi wetu
Imeelezwa kuwa ili lifanyike pambano la kukata mzizi wa fitina kati ya mabondia maarufu nchini, Hassan Mwakinyo na Twaha Kassim ‘Kiduku’ ni lazima mmoja wao afuate uzito wa mwingine na si vinginevyo.
Hayo yameelezwa leo Alhamisi na katibu mkuu wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC), George Silasi akifafanua kuwa Watanzania wanapaswa kulielewa hilo kama kweli wanataka kushuhudia wawili hao wakitupiana na makonde.
“Kama kamisheni ya ngumi za kulipwa hatuwezi kuruhusu pambano ambalo mabondia wanaocheza uzito tofauti wapande ulingoni bila kuzingatia vigezo.
“Mabondia wanapambana wakiwa na uzito sawa sio uzito tofauti aidha kama Mwakinyo ana kilo 69 anatakiwa kupambana na Twaha anapaswa kupanda uzito au kama Twaha mwenye kilo 76 anataka pambano na Mwakinyo ashuke,” alisema Silasi na kuongeza:
“Mimi niwaombe mapromota wa ngumi wawekeze sana kwenye hili pambano kwani ni kubwa na sisi kama kamisheni shauku yetu ni kuona mapambano yanafanyika na mchezo wa ngumi unaendelea kukua.”
Kwa muda mrefu sasa mabondia hao wamekuwa wakitambiana kwenye majukwaa, mitandaoni na kwenye mahojiano yao mbalimbali kabla ya hivi karibuni wote wawili kuonesha nia ya kutaka kuzichapa.
Hata hivyo dau, uzito na mapromota vimetajwa kuwa kikwazo cha kukamilika kwa pambano baina yao mpaka sasa.
Mwakinyo hivi karibuni alinukuliwa kwenye sherehe za Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (Taswa) akisema yuko tayari kwa pambano dhidi ya mpinzani anayetajwa lakini lazima kuwe na makubaliano ya uhakika kuhusu maslahi na si kupigana tu.