Paris, Ufaransa
Klabu ya PSG ya Ufaransa imeamua kuwekeza nguvu kubwa ili kuhakikisha inamsajili mshambuliaji wa Tottenham Hotspur, Harry Kane baada ya kuondoka kwa Lionel Messi.
Messi aliihama timu hiyo hivi karibuni na kujiunga na Miami FC ya Marekani hapo hapo kukiwa na habari kwamba huenda klabu hiyo pia ikakimbiwa na mshambuliaji wake mwingine, Kylian Mbappe.
Kutokana na mazingira hayo vigogo PSG wanahaha kusaka mshambuliaji mwenye hadhi na ndio maana wameamua kumfanya Kane kuwa chaguo lao namba moja katika kuimarisha safu yao ya ushambuliaji.
Messi alitangaza mapema kwamba hatasaini mkataba mpya na PSG baada ya kumaliza mkataba wake ulioishia msimu wa 2022-23 wakati Mbappe ambaye mkataba wake unafikia mwisho msimu ujao wa 2023-24 ametangaza kutoongeza mkataba ingawa anataka kubaki na timu hiyo.
Baada ya kumkosa Messi, PSG wanahofu ya kumkosa Mbappe msimu ujao bila kupata chochote hivyo wapo tayari kumpiga bei kwa wakati huu hali ambayo itawafanya kuwa na tatizo kwenye safu ya ushambuliaji na ndipo jina la Kane lilipoibuka na kufanywa chaguo namba moja.
PSG hata hivyo itakuwa na kazi kubwa ya kuwashawishi mabosi wa Spurs kumuuza mshambuliaji huyo hapo hapo kukiwa na habari kwamba Real Madrid nayo inamtaka hasa baada ya kuondoka kwa Karim Benzema.
Timu nyingine zilizowahi kuhusishwa na mipango ya kumtaka Kane ni Bayern Munich na Man United, wakati Munich wakiwa kimya, Man United wametangaza hivi karibuni kujitoa katika mpango huo.
Kimataifa Kane chaguo namba moja PSG
Kane chaguo namba moja PSG
Read also