Rio de Janeiro, Brazil
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Brazil, Neymar atazikosa fainali za michuano ya soka ya Copa America zitakazofanyika mwakani nchini Marekani kutokana na maumivu ya goti yanayomkabili.
Daktari wa timu ya taifa ya Brazil, Rodrigo Lasmar amethibitisha hilo jana Jumanne ikiwa imepita miezi miwili tangu mchezaji huyo aumie katika mechi ya Brazil dhidi ya Uruguay ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026.
Neymar, nyota wa zamani wa Barcelona na PSG ambaye kwa sasa anaichezea Al Hilal ya Saudi Arabia, aliumia goti la mguu wa kushoto katika mechi hiyo na kufanyiwa upasuaji wiki mbili baadaye.
Fainali za Copa America zitaanza kutimia vumbi Juni 20 hadi Julai 14 na Dk Lasmar ametaka kusiwe na haraka ya kumuwahisha mchezaji huyo kwani kufanya hivyo kunaweza kusababisha tatizo kuwa kubwa zaidi hapo baadaye.
“Ni mapema mno, hakuna sababu ya kukwepa hatua za tiba kwa lengo la kutaka kupona haraka na kujiweka katika hali hatari zaidi, matarajio yetu ni kwamba atajiandaa kurudi uwanjani mwanzoni mwa msimu wa 2024 Ulaya ambao unaanza mwezi Agosti,” alisema Dk Lasmar.
“Tunahitaji kuwa na subira, kuzungumzia kurudi uwanjani kabla ya miezi tisa ni kutaka kuwahisha jambo, hizi ni taratibu za duniani kote kuhusu matatizo ya goti na upasuaji, ni muhimu kuheshimu muda wa kitabibu, muda ambao mwili unahitaji ili kuwa fiti,” alisema Dk Lasmar.
Dk Lasmar alisisitiza kwamba kama hatua husika zitafuatwa, baada ya kuwa katika kipindi kirefu cha kupona, matarajio ni kwamba Neymar anaweza akapona na kucheza kwa mara nyingine kwa kiwango cha juu.
Neymar kwa sasa ndiye mshambuliaji wa timu ya taifa ya Brazil mwenye mabao mengi katika historia ya timu hiyo akiwa amefunga jumla ya mabao 79 katika mechi 129.
Katika fainali za Copa America, Brazil imepangwa Kundi D pamoja na timu za Paraguay, Colombia na timu mojawapo kati ya Costa Rica au Honduras ambazo zinasubiri kucheza Playoff ili kupata mshindi.