Na mwandishi wetu
Simba imefunguka kuwa ipo kwenye mikakati ya kumsajili kwa ajili ya msimu ujao kiungo mshambuliaji, Hassan Dilunga anayeendelea kujifua na kikosi cha timu hiyo kwa sasa.
Dilunga ameonekana wiki hii mazoezini baada ya kuwa nje ya uwanja kwa zaidi ya mwaka akiuguza majeraha ya goti aliyoripotiwa kuyapata mwezi Februari, mwaka jana.
Simba kwa sasa inajiandaa na mechi za hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika lakini Dilunga hakujumuishwa kwenye usajili wa timu hiyo msimu huu baada ya kumalizika kwa mkataba wake msimu uliopita.
Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally amesema Dilunga ni mchezaji mzuri na anachohitaji ni utimamu wa mwili pekee kwa sasa, kisha wataangalia la kufanya ili awatumikie kwa mara nyingine kuanzia msimu ujao.
“Dilunga alikuwa nje ya uwanja kutokana na majeraha aliyokuwa nayo, lakini sasa amerudi kama mlivyoona, kiwango chake kinafahamika, kinachoangaliwa sasa nio utimamu wake wa mwili na arejee sawasawa kisha tutaangalia namna ya kuwa naye tena msimu ujao,” alisema Ally.
Dilunga aliyewahi kuzitumikia Yanga na Ruvu Shooting, alitua Simba mara ya kwanza msimu wa 2018-19 baada ya kuonesha kiwango kikubwa akiwa na Mtibwa Sugar ya Morogoro.