Na mwandishi wetu
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu NBC, Yanga wamefanikiwa kunyakua pointi tatu muhimu mbele ya Mashujaa baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mechi iliyopigwa Alhamisi hii kwenye dimba la Azam Complex, Dar es Salaam.
Haikuwa rahisi kwa Yanga kutoka na ushindi katika mechi hiyo kwani baada ya kupambana timu hiyo iliandika bao la kwanza dakika ya 45, bao lililofungwa na Maxi Nzengeli ambaye sasa anakuwa amefikisha mabao manane.
Iliwachukua dakika 20 baada ya kuanza kipindi cha pili kwa Mashujaa kutoka mkoani Tabora kupata bao la kusawazisha lililofungwa na Emmanuel Mtumbuka.
Bao hilo ambalo lilishangiliwa kwa nguvu na mashabiki wa Mashujaa na kuibua matumaini ya timu hizo kugawana pointi lakini zikiwa zimebakia dakika nne mpira kumalizika, Mudathir Yahya alifunga bao na kuiwezesha Yanga kutoka na pointi tatu muhimu.
Kwa ushindi huo Yanga sasa imejituliza kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 37 ikiiacha Azam FC inayoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi sita wakati Simba inayoshika nafasi ya tatu ina pointi 29.
Simba Ijumaa hii itakuwa mwenyeji wa Azam FC kwenye mechi nyingine ya ligi hiyo itakayopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
Soka Yanga yawaadhibu Mashujaa jioni
Yanga yawaadhibu Mashujaa jioni
Read also
