Na mwandishi wetu
Saido Ntibazonzika ameendelea kuthibitisha umuhimu wake katika kikosi cha Simba baada ya Jumatano hii kufunga mabao mawili na kuiwezesha timu yake kutoka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Mbeya City.
Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu NBC iliyopigwa Jumatano hii usiku kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, mshambuliaji huyo aliyetupiwa virago Yanga na kutimkia Geita Gold kabla ya kusajiliwa na Simba katika usajili wa dirisha dogo, alianza kuziona nyavu katika dakika ya 11 ya mchezo akiitumia vizuri pasi ya Clatous Chama au Mwamba wa Lusaka.
Furaha ya Simba hata hivyo ilidumu kwa dakika nne tu kwani katika dakika ya 15, Mbeya City walisawazisha bao hilo kupitia kwa Richardson ambaye aliinasa pasi ya Salum na kuandika bao lililotosha kuwanyamazisha mashabiki wa Simba.
Dakika mbili baada ya mapumziko, Ntibazonkiza kwa mara nyingine aliiongezea Simba bao la pili kabla Pape Sakho hajaandika bao la tatu dakika nane baadaye.
Mbeya City hawakuonekana kutetereka licha ya mabao hayo na hawakucheza kwa kujihami zaidi kwa hofu ya kufungwa mabao mengine, badala yake walipambana na kutengeneza nafasi kabla ya kupata bao la pili katika dakika ya 79.
Kwa matokeo hayo Simba inazidi kujiimarisha katika nafasi ya pili huku ikiendelea kuifukuzia Yanga inayoshika usukani wa ligi hiyo ikiwa na pointi 53 wakati Simba imefikisha pointi 47 na timu zote hizo zimecheza mechi 20 hadi sasa.
Soka Simba yaikanyaga Mbeya City
Simba yaikanyaga Mbeya City
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
