Na mwandishi wetu
Rais wa Fifa, Gianni Infantino na Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Patrice Motsepe pamoja na marais wa vyama vya soka maeneo mengine watakuwa jijini Dar es Salaam kushuhudia mechi ya uzinduzi wa African Football League (AFL) kati ya Simba na Al Ahly.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Imani Kajula alisema watakuwa katika mechi hiyo ya ligi mpya inayoshirikisha timu nane za Afrika kwa msimu huu.
Simba itaanza michuano hiyo kwa kuumana na mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly ya nchini Misri kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam Oktoba 20.
Kajula aliyasema hayo leo Jumatano katika mkutano na waandishi wa habari huku akiishukuru Serikali ya Tanzania kwa maboresho makubwa waliyoyafanya kwenye Uwanja wa Mkapa kwa ajili ya michuano hiyo.
“Rais wa Fifa atakuwepo, Rais wa CAF atakuwepo na marais wa vyama vya soka vya maeneo mengine pia tunajua kutakuwa na watu mbalimbali kutoka mikoani na jana (juzi) tulikuwa na mkutano na AirTanzania ili kupata punguzo la bei ya tiketi kwa mashabiki wa Simba kutoka mikoani,” alisema Kajula.
Alisema lengo ni kujaza watu 60,000 na wanatarajia tiketi zitauzwa kwa haraka hivyo watu wanunue kwa haraka kwa sababu wanatarajia watu wengi kutoka nje ya Dar es Salaam na kuhusu tiketi za makundi zitaendelea kuwepo.
“Tunaishukuru serikali kwa matengezo makubwa ambayo imeyafanya kwenye Uwanja wa Mkapa ambao utaenda kufungua mashindano haya makubwa barani Afrika lakini pia sisi tumetoa mchango kiasi kufanikisha hili,” alisema Kajula.
Naye Meneja wa Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema mechi hiyo ya uzinduzi itaanza saa 12:00 jioni kwenye Uwanja wa Mkapa na timu yao tayari imeingia kambini baada ya mapumziko ya mchezo uliopita walipopata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Singida Fountain Gate.
“Kuhusu wachezaji walioitwa timu za taifa tunaendelea na mazungumzo na mashirikisho ili wachezaji walioitwa wawahi kurudi ili tujiandae kwa ubora zaidi.
“Viingilio tumepanga kwa kuangalia hali za watu wetu pamoja na hadhi ya michuano hii; Platinum Sh 200,000, hatutakuwa na VIP A sababu jukwaa limechukuliwa na Fifa na CAF, VIP B ni Sh 40,000, VIP C Sh 30,000, viti vya machungwa Sh 10,000 na mzunguko Sh 7,000. Tiketi tayari zimeanza kuuzwa vituoni,” alisema Ally.