Miami, Marekani
Kiungo wa Aston Villa na timu ya taifa ya England, Morgan Rogers amesema mshambuliaji Erling Haaland wa Norway anaweza kuwa ni mchezaji asiyezuilika lakini anaamini wanapaswa kuzuia mipira isimfikie.
England na Norway zitaumana Jumamosi katika mechi ya robo fainali ya Kombe la Dunia 2026 huku Rogers ambaye anacheza nafasi ya kiungo mshambuliaji na winga akiamini kuzuia njia zinazofanya mipira imfikie Haaland ni jambo muhimu katika kuweka hai ndoto za England kusonga mbele.
Haaland ambaye pia ni mshambuliaji wa Man City ndiye aliyefanya kazi kubwa hadi timu hiyo ikawatoa Brazil katika fainali za Kombe la Dunia na sasa inasubiriwa kuona kama atafanya hivyo dhidi ya England.
Mafanikio ya Haaland yameonekana katika klabu yake ya Man City ambapo ameibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu England mara tatu katika misimu minne iliyopita ukiwamo msimu wa 2025-26 ambao alimaliza na mabao 27 katika mechi 35.
Hadi sasa ameshaifungia Norway mabao saba hadi timu hiyo kufikia hatua ya robo fainali akiwa katika kiwango bora ambacho kinawaweka katika wakati mgumu England wakati timu hizo zikisubiri kuumana Jumamosi.
“Wana mmoja wa washambuliaji bora duniani, anapokuwa uwanjani lolote linaweza kutokea, huwezi kushangaa Haaland akifunga mabao mawili na timu yao kupata ushindi, amefanya hivyo mara nyingi katika maisha yake ya soka na anaendelea kufanya hivyo,” alisema Rogers.
Rogers alisema hana uhakika kama kuna aliyewahi kumzuia Haaland lakini wao England watajaribu kufanya hivyo japo alikiri kuwa mchezaji huyo yuko katika kiwango bora na anafanya mambo ambayo huwezi kuamini.
Rogers pia alisema Norway kwa ujumla ni timu nzuri na si Haaland peke yake kwani wana wachezaji wengine wazuri ambao wamekuwa wakicheza nao mara kwa mara katika Ligi Kuu England.
Rogers na mchezaji mwenzake Ezri Konsa walikuwa katika kikosi cha Villa ambacho kiliifunga Man City mara tatu huku Haaland akishindwa kupata bao.
Alifafanua kuwa ni kweli wamewahi kumdhibiti Haaland katika mechi zao na City lakini alikiri kuwa kila mechi ina utofauti wake na mchezaji huyo anaweza kubadili mambo hivyo ni lazima wawe makini kwani pia mechi hiyo itakuwa ngumu.
