Na mwandishi wetu
Rais wa TFF, Wallace Karia, amesema kuwa hivi sasa malengo yao ni kuupumzisha Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Dar es Salaam kwa kuupunguzia matumizi ili uendelee kuwa bora.
Alisema kutokana na ubora wake ndio sababu Tanzania ilipata nafasi ya kuzindua michuano mikubwa ya Afrika Football League, tukio ambalo ni kubwa na la kihistoria na uwanja haukuharibika.
“Miundombinu ni jambo ambalo lilikuwa na changamoto sana, sasa hivi viwanja mmeona vinapendeza lakini Uwanja wa Mkapa ni uwanja wa serikali. Sisi tunachoangalia ni kuhakikisha uwanja hatuuzidishii matumizi.
“Ikiwezekana kwenye ligi zetu ichezwe mechi ya Simba na Yanga tu, kuhusu ligi mechi zinazoihusu Simba au Yanga zitachezwa sehemu nyingine, ila wanapocheza wao wenyewe sawa na hata timu ya taifa tunataka tuangalie sehemu nyingine ya kucheza ili uwanja upumue,” alisema Karia.
Alisema kutokana na baadhi ya nchi kutokuwa na viwanja vyenye sifa zinazokidhi viwango vya CAF kimbilio lao limekuwa Uwanja wa Mkapa ambao umekuwa msaada kwa mataifa mengi.
“Wiki iliyopita kulikuwa na mechi nne mfululizo, Gambia dhidi ya Burundi, Burundi na Gabon, Gambia na Ivory Coast kisha Tanzania dhidi ya Morocco lakini uwanja bado ni mzuri tu.
“Wiki hii Simba wamecheza hapo, Desemba Mosi watacheza Al Hilal na Esperance wakati Desemba 2 Yanga watacheza na Al Ahly na bado uwanja unasimama katika viwanja bora Afrika,” alisema Karia.