Na mwandishi wetu
Imebainika kuwa nyota wawili wa Azam FC, Prince Dube na Yahya Zayd watakuwa nje ya uwanja kwa muda wiki tatu kila mmoja kutokana na majeraha waliyoyapata hivi karibuni.
Wawili hao waliumia na kufanyiwa mabadiliko kwenye mechi yao ya mwisho ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Singida Big Stars waliyoshinda mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Akizungumza na GreenSports, Ofisa Habari wa Azam, Thabiti Zakaria alisema baada ya vipimo vya kina chini ya jopo la madaktari wao walibaini kuhusu majeraha ya wachezaji wao hao ambao wataanza kuukosa mchezo wa kesho wa ligi dhidi ya Dodoma Jiji.
“Dube anasumbuliwa na majeraha ya nyonga na Yahya yeye ameibainika amechanika kiraba (meniscus) kinachokuwa katikati ya goti, kinacholiimarisha lisikwaruzane. Kiraba hicho pia huwezesha goti kufanya kazi vizuri kwa maana ya kukunja na kukunjua,” alisema Zakaria.
Ameeleza kuwa wachezaji hao kwa sasa wanaendelea na programu ya kutibu majeraha yao chini ya uangalizi wa mtaalamu wa tiba za viungo wa timu hiyo, Joao Rodrigues.