Na mwandishi wetu
Simba imezidi kutanua makucha baada ya Shirikisho la Kimataifa la Takwimu na Historia za Soka (IFFHS) kutoa orodha ya timu 20 za Afrika zinazoongoza kwa ubora kwa kipindi cha miezi 12 iliyopita.
Kwa mujibu wa takwimu hizo zilizotolewa leo, Simba inashika nafasi ya 11 Afrika na ya 131 duniani. Takwimu hizo hupangwa kulingana na matokeo ya klabu husika kwenye ligi ya ndani, makombe ya ndani na mashindano ya kimataifa.
Katika mechi za nyumbani kwa maana ya ligi Simba imekuwa katika kiwango bora kwani ni miongoni mwa timu tatu ambazo hazijapoteza mchezo wowote mpaka sasa.
Takwimu hizo zimekuja wakati Simba ikiongoza Ligi Kuu ya NBC kwa pointi 13 katika michezo mitano, ikiwa imepata sare moja na haijafungwa huku ikiwa ndiyo timu pekee iliyofungwa mabao machache, mabao mawili.
Pia, katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba imetanguliza mguu mmoja kutinga hatua ya makundi ya ligi hiyo baada ya wiki iliyopita ilipokuwa ugenini Angola kuifunga mabao 3-1 Primiero de Agosto kabla ya mechi ya marudiano itakayopigwa Jumapili hii jijini Dar es Salaam.
Katika orodha ya Afrika, Al Ahly ya Misri inaongoza kwenye 10 Bora ikifuatiwa na Wydad Casablanca, Zamalek SC, Atlético de Luanda, Mamelodi Sundowns, CR Belouizdad, Pyramids FC, RS Berkane, Raja Casablanca na ES Sétif.
Timu zinazofuatia ni Simba, JS Saoura, Orlando Pirates, Esperance, TP Mazembe, Al Masry, Al Hilal Omdurman, Al Ahli Tripoli, JS Kabylie na Red Arrows FC.
Soka Simba ya 11 kwa ubora Afrika
Simba ya 11 kwa ubora Afrika
Read also