Na mwandishi wetu
Vinara wa Ligi Kuu NBC, Yanga wataanza kuumana na ASAS Télécom ya Djibout kwenye hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Simba ikisubiri kucheza raundi ya pili na mshindi baina ya African Stars ya Namibia au Power Dynamos ya Zambia.
Shirikisho la Soka Afrika (Caf) leo Jumanne limepanga droo hiyo pamoja na ile ya Kombe la Shirikisho Afrika ambako Tanzania inawakilishwa na timu za Azam, Singida Fountain Gate na JKU.
Simba itaanzia hatua ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa kwa kuwa ipo katika kundi la timu 10 bora barani Afrika.
Yanga ambayo itaanzia ugenini dhidi ya ASAS, ikifanikiwa kuvuka hatua hiyo, itapepetana na mshindi baina ya mabingwa wa Congo, AS Otoho na El Merreikh ya Sudan iliyomaliza nafasi ya pili kwenye ligi chini ya Al Hilal.
KMKM kutoka visiwani Zanzibar yenyewe itaanza kwa kuumana na St. George ya Ethiopia na ikivuka hapo ni uso kwa uso na mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa, Al Ahly.
Kwenye Kombe la Shirikisho, Azam imepangwa kucheza dhidi ya Bahir Dar Kenema waliomaliza nafasi ya pili kwenye Ligi ya Ethiopia na mshindi baina yao atapambana na Club Africain ya Tunisia.
Na Singida FG inayoshiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza itacheza na ndugu zao JKU kutoka Zanzibar, kisha mshindi atavaana na Future FC ya Misri.
Mechi za mkondo wa kwanza za hatua ya awali za Ligi ya Mabingwa zitachezwa kati ya Agosti 18 mpaka 20 wakati marudiano zikitarajiwa kupigwa Agosti 25, mpaka 27, mwaka huu.
Kimataifa Wapinzani wa Yanga, Simba CAF hadharani
Wapinzani wa Yanga, Simba CAF hadharani
Read also