Doha, Qatar
Richarlison amefunga mabao mawili na kuiwezesha Brazil kutoka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Serbia katika mechi ya Kundi G ya fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea Qatar.
Katika mechi hiyo iliyochezwa Alhamisi hii usiku, Serbia walioonekana kuwa wagumu dhidi ya mabingwa hao wa dunia mara tano, hatimaye walianza kusalimu amri katika dakika ya 62 baada ya Richarlison kuandika bao la kwanza lililotokana na mpira uliopigwa na Vinicius Junior na kuokolewa na kipa wa Serbia, Vanja Milinkovic-Savic kabla ya kumkuta mfungaji.
Richarlison ambaye pia ni shambuliaji wa Tottenham alikamilisha idadi ya mabao ya Brazil katika dakika ya 73 akiandika bao la pili kwa timu yake baada ya kuitumia pasi ya nyota wa Real Madrid, Vinicius Junior ya mpira wa juu ambao aliuwahi kwa juu na kufumua shuti la mguu wa kulia lililojaa wavuni.
Mabao hayo yalionekana kuivuruga Serbia ambayo kipindi cha kwanza ilionekana kama kujihami zaidi na iliyocheza kwa dhamira ya kuvuruga mipango ya Brazil zaidi kwani haikuweza kufanya mashambulizi yoyote ya maana kwa Brazil waliocheza kwa utulivu wa hali ya juu na kufanikiwa kuutawala vyema mchezo hadi kupata ushindi huo muhimu katika mechi yao ya kwanza.
Ushindi huo ambao umeanza kubeba matumaini iliyopewa timu hiyo kubeba taji la dunia, umekuja na hali ya wasiwasi kwa timu hiyo baada ya nyota wa Brazil Neymar aliyeshiriki vizuri katika bao la kwanza la timu hiyo kuumia enka katika mguu wa kulia na kulazimika kutoka uwanjani dakika ya 80.
Ukiacha Richarlison ambaye ndiye aliyefunga mabao ya Brazil, kivutio kingine kwa timu hiyo alikuwa ni kiungo wa Man United, Casemiro ambaye alilitawala vyema dimba la kati.
Mechi za leo Kombe la Dunia
Kundi A
Qatar v Senegal
Uholanzi na Ecuador
Kundi B
Wales v Iran
England v Marekani
