Njeru, Uganda
Timu ya vijana chini ya miaka 15 ya Zanzibar imetwaa taji la Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) baada ya kuwabwaga wenyeji Uganda kwa penalti 4-3.
Katika mechi hiyo ya fainali iliyopigwa Alhamisi hii jioni, timu hizo zilipigiana penalti baada ya sare ya bao 1-1 katika dakika 90 na Zanzibar kubebwa na umahiri wa kipa wake, Mahir Omar aliyeokoa mikwaju miwili ya penalti.
Katika dakika 90 za kawaida, Zanzibar ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 19 ya mchezo huo, bao lililofungwa na Lukman Omar.
Uganda au The Rhinos walipambana na kufanikiwa kusawazisha katika dakika ya 30 mfungaji akiwa ni Ibra Ssegabala na kufanya matokeo kuwa sare ya bao 1-1 hadi dakika 90 zinamalizika.
Waliofunga penalti zao kwa Uganda ni Ssebagala, Enock Bagenda na Richard Okelo wakati kwa Zanzibar waliofunga ni Lukman, Saleh Mbarouk, Hassan Idd na Adam Shanan.
Waliokosa penalti kwa upande wa wenyeji Uganda ni Ronald Kigoye na Ratib Gulanyango wakati kwa Zanzibar aliyekosa ni Fahad Hassan.
Ushindi huo unaifanya timu ya Zanzibar kuwa ya pili kubeba taji la michuano hiyo iliyoanzishwa mwaka 2019 nchini Eritrea ambapo Uganda ndio walioibuka vinara katika fainali hizo.
Katika mechi ya kusaka nafasi ya tatu, timu ya Tanzania Bara iliibuka kinara baada ya kuichapa Sudan Kusini bao 1-0, mfungaji wa bao hilo pekee akiwa ni Seleman Kaniki.
Zanzibar: Zanzibar: Mahir Amour, Ashraf Othman, Mwinyi Hassan, Abdulnassir Makarani, Lukman Omar, Mohamed Nasser, Saleh Mbarouk, Hafidh Salmin, Mohamed Mohamed, Hussein Mbegu na Hassan Iddi
Uganda: Edrisah Waibi, Samuel Mubiru, Ratib Gulanyago, Abubakali Walusimbi, Simon Wanyama, Richard Okello, Pius Oyirwoth, Owen Mukisa, Ibra Ssebagala, Ronald Kigoye na Enock Bagenda
Baada ya mechi ya fainali, wachezaji Owen Mukisa wa Uganda alipewa tuzo ya MVP na Lazarus Peter George wa Sudan Kusini alipewa tuzo ya mfungaji bora kwa mabao manane aliyofunga.
Kimataifa Zanzibar yabeba taji la Cecafa U-15
Zanzibar yabeba taji la Cecafa U-15
Related posts
Read also