Na mwandishi wetu, Unguja, Zanzibar
Yanga imetoa dozi ya mabao 5-0 kwa Jamhuri katika mechi ya Kombe la Mapinduzi, ushindi ambao uliambatana na utambulisho wa usajili mpya wa Augustin Okrah ambaye aliibua mjadala siku za karibuni.
Okrah mmoja wa wafungaji wenye mabao mengi katika Ligi Kuu Ghana akiwa amezifumania nyavu mara nane, anajiunga na Yanga akiwa bado yumo katika kumbukumbu za kukipiga na mahasimu wa Yanga, Simba.
Kiasi cha pesa kilichotumika kumsajili mchezaji huyo hakijawekwa wazi ingawa habari tulizoziripoti awali kutoka chanzo kimoja nchini Ghana, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 amesajiliwa kwa Dola 150,000 zaidi ya Sh milioni 375.
Okrah maarufu kama Magic Okrah alitambulishwa wakati wa mapumziko kwa staili ya mfano wa mazingaombwe akioneshwa kama ameibukia kimaajabu uwanjani hapo na baadaye aliwasalimia mashabiki na kuwapa zawadi ya jezi alizokuwa akizirusha jukwaani.
Usajili wa Okrah hata hivyo umekuwa mjadala katika siku za karibu baadhi wakitilia shaka kama kweli Yanga ilikuwa na mpango wa kumsajili mshambuliaji huyo na wengine wakihoji nafasi yake katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Nje ya utambulisho wa Magic Okrah, Yanga walitumia dakika 45 za kwanza kuisambaraisha Jamhuri na kuweka rekodi ya kufunga mabao mengi katika mechi ya Kombe la Mapinduzi msimu huu wa 2023-24.
Mabao ya Yanga yalifungwa na Crispin Ngushi aliyefunga mawili dakika za 10 na 17, Kibwana Shomari aliyefunga bao dakika ya 23 na Clement Mzize na Skudu Makudubela waliofunga dakika za 36 na 45.
Kocha Miguel Gamondi baada ya kupata mabao matano ya kipindi cha kwanza aliwatoa wachezaji kadhaa wa kikosi cha kwanza akiwamo Kibwana Shomari, Clement Mzize na wengineo na kuingiza damu changa hali iliwayofanya Jamhuri kupata nguvu lakini hawakuweza kutumia nafasi hiyo kubadili matokeo ya mchezo huo.
Ushindi huo wa Yanga pia unakuwa zawadi ya Mwaka Mpya wa 2024 kwa mashabiki wake kwani ulipatikana takriban saa moja na nusu kabla ya kuuaga mwaka 2023.
Katika mechi nyingine iliyochezwa awali Jumapili hii, timu za KVZ na Jumus zilimaliza dakika 90 kwa sare ya bao 1-1.
Soka Yanga yaipiga Jamhuri 5-0, yamtambulisha Okrah
Yanga yaipiga Jamhuri 5-0, yamtambulisha Okrah
Read also
