Na mwandishi wetu
Yanga iko kamili, haina majeruhi, itaondoka keshokutwa alfajiri kuelekea Sudan kwa ajili ya mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal.
Yanga imeeleza kuwa inatarajia kutua nchini humo majira ya saa 6.45 tayari kwa ajili ya mechi hiyo itakayopigwa Jumapili hii Uwanja wa Al Hilal, Khartoum baada ya ile ya awali iliyopigwa Uwanja wa Mkapa wikiendi iliyopita na kuisha kwa sare ya 1-1.
Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe ameeleza kwamba wataondoka majira hayo na Shirika la Ndege la Ethiopia wakipitia Addis Ababa kabla ya kutua Khartoum wakiwa na kikosi kamili ambacho mpaka hakina majeruhi.
“Kwanza tumekuwa na kambi nzuri baada ya mapumziko ya siku moja na timu kurejea mazoezini Jumatatu na kuendelea na kubwa la kushukuru mpaka sasa hakuna ripoti ya mchezaji aliyepata majeruhi.
“Na kuhusu safari, timu itasafiri siku ya Jumamosi (kesho) alfajiri majira ya saa 10, tutapitia Addis Ababa na kisha Khartoum ambapo tutatua majira kama ya saa 5.45 lakini huku itakuwa saa 6.45 mchana,” alisema Kamwe.
Pia ofisa huyo alieleza namna benchi la ufundi la timu hiyo na wachezaji wanavyotambua juu ya hisia za mashabiki wanaodhani kuwa hawataweza kufuzu kutokana na matokeo ya awali, hivyo wameahidi kupambana kuhakikisha wanarejesha amani kwa mashabiki na kufuzu hatua ya makundi.
“Timu ina ari na morali kubwa ya kwenda kufanya vizuri Sudan, benchi la ufundi linatambua mtihani mkubwa tulionao na tumesikia maoni ya mashabiki na wanachama kwa kuwa hayakuwa matokeo ya kufungwa lakini kwa uhalisia wa mechi za nyumbani na ugenini wanahisi hakuna nafasi ya kufanya vizuri ugenini.
“Lakini benchi la ufundi na wachezaji wamepokea hisia za mashabiki na wanachosisitiza ni mashabiki waendelee kuwa na timu maana bado tuna dakika 90 nyingine na kwa maandalizi tuliyonayo bado tuna nafasi ya kufanya vizuri na kucheza hatua ya makundi,” alisema Kamwe.
Soka Yanga kamili yaifuata Al Hilal Sudan
Yanga kamili yaifuata Al Hilal Sudan
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
