London, England
Leeds United jana Jumatatu ilimfuta kazi kocha Jesse Marsch ikiwa ni siku moja baada ya timu hiyo kufungwa bao 1-0 na Nottingham Forest katika mechi ya Ligi Kuu England (EPL).
Uamuzi wa kumfukuza Marsch ambaye hajamaliza hata mwaka na Leeds, umekuja baada ya timu hiyo kucheza mechi saba mfululizo za EPL bila kushinda hata moja huku ikiwa nafasi ya 17 katika ligi hiyo.
Leeds ambayo mara ya mwisho kupata ushindi katika EPL ilikuwa Novemba mwaka jana, msimu uliopita ilimaliza ligi ikiwa nafasi ya 17 na Februari mwaka jana ilimtimua kocha Marcelo Bielsa na majukumu yake kupewa Marsch.
Taarifa ya klabu hiyo ilieleza kuhusu kumtimua Marsch, “tungependa kumshukuru Jesse na wasaidizi wake kwa juhudi zao na tunamtakia kila la heri kwa siku zijazo.”
“Taratibu za kumteua kocha mpya zinaendelea na tutaendelea kuwapa mashabiki taarifa nzima kwa kila kinachojiri katika siku chache zijazo,” ilifafanua taarifa hiyo.
Marsch aliyewahi kuzinoa timu za RB Leipzig, New York Red Bulls na Red Bull Salzburg hapo kabla, aliinusuru Leeds na janga la kushuka daraja msimu uliopita lakini msimu huu umekuwa mgumu kwake.
