Na mwandishi wetu
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameipongeza Yanga kwa kufuzu nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika huku akiitakia maandalizi mema dhidi ya wapinzani wao, Marumo Gallants ya Afrika Kusini.
Yanga ilitinga hatua hiyo baada ya kuiondosha Rivers United ya Nigeria kwa jumla ya mabao 2-0. Mechi ya kwanza Yanga ilishinda kwa mabao 2-0 ikiwa ugenini kabla ya suluhu ya mechi ya pili kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Rais Samia ameipongeza timu hiyo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter akiwapongeza kwa kuandika historia akiwataka waifanyie kazi, maradufu hamasa yake ya kutoa Sh milioni 10 kwenye kila bao watakalofunga kwenye michuano hiyo.
“Pongezi kwa klabu ya Yanga kutinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho, na kila la heri katika maandalizi mliyoanza sasa kwa mchezo ujao. Mmeandika historia jalili, mmetuheshimisha sana, hamasa
yangu inaendelea na sasa imeongezeka kaifanyieni kazi,” aliandika Rais Samia.
Hii ni mara ya kwanza Yanga kutinga hatua hizo za juu kwenye michuano hiyo ya kimataifa ikiweka historia nchini baada ya kushiriki kwa miaka mingi bila mafanikio.
Yanga itaanza kutupa karata yake ya kwanza dhidi ya Marumo Mei 10, mwaka huu ikiwa nyumbani kabla ya kurudiana Mei 17 nchini Afrika Kusini.
Gallants yenyewe ilitinga hatua hiyo baada ya kuindosha Pyramids ya Misri kwa jumla ya mabao 2-1. Mchezo wa kwanza walitoka sare ya bao 1-1 ugenini na mchezo wa pili walishinda kwao bao 1-0.
Nusu fainali nyingine ya michuano hiyo itazikutanisha USM Alger ya Algeria dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast.
Kimataifa Rais Samia aipongeza Yanga
Rais Samia aipongeza Yanga
Read also