Manchester England
Kocha wa Man United, Michael Carrick amempongeza kiungo wake Bruno Fernandes (pichani) kwa ushawishi wake kwenye timu na kiwango bora alichokionesha msimu huu.
Fernandes, 31, ambaye anatajwa kuwania tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka, tangu akatae ofa ya kwenda kucheza soka Saudi Arabia majira ya kiangazi mwaka jana, amekuwa na soka la kuvutia akitoa asisti 18 na kuipaisha timu hiyo katika tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Katika asisti Fernandes hadi sasa amezidiwa asisti mbili na Kevin de Bruyne na Thierry Henry kwa msimu mmoja wa ligi kuu na yumo katika orodha ya wachezaji wanaowania tuzo za PWA na FWA mwishoni mwa msimu.
Alipoulizwa amewezaje kumfanya kiungo huyo wa Ureno kuwa katika ubora wake, Carrick alisema kwamba hakuna zaidi ya kumpa nafasi ya kuonesha kiwango chake.
“Kama ilivyo kwa wachezaji wengine nafikiri tunajitahidi kuweka mazingira na mfumo wa timu kwa lengo la kumpa kila mmoja nafasi ya kujitoa katika ubora kwa jambo hilo,” alisema Carrick.
Carrick hata hivyo alisema ni kweli kwamba kuna mipaka kwa kila mmoja kwa namna anavyojitoa kwa faida ya timu lakini kwake anapenda kumuona Bruno akiwa na uhuru kiasi fulani katika eneo la kiungo mshambuliaji.
“Ni dhahiri amekuwa akicheza kwa ajili ya timu na ana majukumu makubwa katika timu na nafikiri alifanya hivyo kwa ubora hasa Jumamosi katika mechi na Chelsea, akiwa na mpira na hata akiwa hana mpira pamoja na kazi ya ulinzi aliifanya vizuri,” alisema Carrick.
Katika mechi na Chelsea, Man United ilishinda kwa bao 1-0 na kwa mujibu wa Carrick, Fernandes alikuwa na majukumu makubwa lakini kiujumla ni mchezaji mzuri, mbunifu, ana akili ya soka, ana mchango mkubwa na ni mwenye ushawishi mkubwa kwenye timu.
