Rabat, Morocco
Timu ya wanawake ya Afrika Kusini ‘Banyana Banyana’ imeibuka vinara katika fainali za Soka la Wanawake Afrika (Wafcon) baada ya kuilaza Morocco mabao 2-1 katika mechi iliyopigwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdellah mjini Rabat, Morocco.
Shujaa wa Banyana Banyana katika mechi hiyo alikuwa ni mshambuliaji Hildah Magaia anayecheza soka nchini Korea Kusini aliyefunga mabao yote mawili kabla Rosella Ayane hajaifungia Morocco bao pekee la kufutia machozi.
Timu hizo ziliuanza mchezo kwa kushambuliana kwa zamu lakini hadi mapumziko hakuna timu iliyopata bao hadi kipindi cha pili pale Hildah alipoandika bao la kwanza kwa Banyana Banyana katika dakika ya 63 akiujaza mpira wavuni kiulaini baada ya kazi kubwa iliyofanywa na Jermaine Seoposenwe aliyewazidi ujanja mabeki wawili kabla ya kumpasia mfungaji.
Bao la pili la Banyana Banyana lilitokana na krosi ya Karabo Dhlamini iliyotokea upande wa kushoto na kumkuta Hildah ambaye aliitumia vyema kuwanyamazisha mashabiki wa Morocco waliokuwa wakishangilia kwa nguvu wakiwa na matumaini ya timu yao kusawazisha bao.
Mabao hayo hata hivyo hayakuwakatisha tamaa Morocco ambao walipambana na zikiwa zimebaki dakika 10 mpira kumalizika, Tagnaout alitumia udhaifu wa safu ya ulinzi ya Banyana Banyana na kumuunganishia pasi Rosella aliyeipatia Morocco bao lao pekee katika mechi hiyo.
Mbali na taji hilo, kipa wa Banyana Banyana, Andile Dlamini ametwaa tuzo ya kipa bora wa mwaka Afrika kwa upande wa wanawake, tuzo ambayo ameitoa zawadi kwa familia yake kwa namna ambavyo wamekuwa wakimpa ushirikiano.
Nyota wa mabao wa timu hiyo, Hildah naye ametwaa tuzo ya nyota wa mchezo huo na kupata tuzo ya mfungaji bora akiwa amefungana kwa mabao na nahodha wa Morocco, Ghizlane Chebbak na Rasheedat Ajibade wa Nigeria wakati Bayana Banyana imetwaa tuzo ya timu bora ya mwaka kwa wanawake Afrika kila mmoja akiwa na mabao matatu.
