Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha amesema kiwango kilichooneshwa na wachezaji wake kwenye ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Jwaneng Galaxy, kimeonesha mwanga mzuri na kumpa matumaini ya kufanya vizuri kwenye hatua ya robo fainali.
Alisema ulikuwa mchezo mzuri na anawapongeza wachezaji wake kwa kupambana na kujituma na kufanya kile ambacho amewatuma mazoezini na kufanikiwa kuingia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kishindo.
“Niwapongeze wachezaji wamepambana sana, mashabiki wamejitokeza kwa wingi kusapoti timu yao, tulifanya maandalizi mazuri kwa kuzingatia mambo muhimu, mbinu, ufundi, kisaikolojia kwa vijana wangu na kuwasisitiza katika kupambana.
“Wamefanya kile nilichowapa katika uwanja wa mazoezi kwa kushinda idadi kubwa ya mabao 6-0, kwangu tungeshinda bao 1-0 pia ingekuwa vizuri kwa kuwa tulihitaji kufuzu hatua nyingine,” alisema Benchikha.
Aliongeza kuwa baada ya mechi hiyo wanaenda kujipanga kwa ajili ya mechi zilizopo mbele yao zikiwemo za Ligi Kuu NBC kabla ya kufanya maandalizi ya michezo ya hatua ya robo fainali.
