Na Hassan Kingu
Mabao ya Augustine Okrah na Stephen Aziz Ki, yameifanya miamba ya soka nchini Simba na Yanga kutoka uwanjani leo kwa sare ya bao 1-1 katika mechi ya Ligi Kuu ya NBC iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Katika mechi hiyo maarufu Dar Derby iliyotawaliwa na ubabe, ushindani mkali na ufundi wa hapa na pale, Simba ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 15 ya mchezo huo, bao lililotokana na ushirikiano wa Okrah na Clatous Chota Chama au Mwamba wa Lusaka.
Okrah alimuunganishia pasi Chama ambaye akiwa katikati ya mabeki wa Yanga aligeuka kwa haraka na kumpenyezea mpira wa chini chini Okrah ambaye aliambaa nao kabla ya kufumua shuti na mpira kumpita miguuni kipa wa Yanga, Djigui Diarra.
Sekunde chache kabla ya timu kwenda mapumziko, Aziz Ki aliwainua vitini mashabiki wa Yanga baada ya kuipatia timu hiyo bao la mpira wa adhabu ambayo iliyolewa na mwamuzi Ramadhan Kayoko baada ya Aziz Ki kuchezewa rafu na Chama nje ya eneo la 18.
Aziz Ki alidhihirisha uwezo wake wa kuitumia mipira ya adhabu, alimchungulia kipa wa Simba, Aishi Manula, akarudi nyuma kidogo na kufumua shuti la mguu wa kushoto lililojaa wavuni kwa juu upande wa kulia wa Manula ambaye juhudi zake za kudhihirisha U-Air Manula wake hazikuweza kufua dafu mbele ya shuti hilo kwani licha ya kuufuata mpira lakini alipishana nao akiwa angani.
Bao hilo lilituliza munkari wa mashabiki wa Yanga na kuwaweka katika hali ya mshangao mashabiki wa Simba hali iliyosababisha kipindi cha pili kianze kidogo katika hali ya utulivu kuanzia kwa wachezaji hadi mashabiki majukwaani.
Simba ndio waliokuwa wa kwanza kulisumbua lango la Yanga katika dakika ya kwanza tu ya mchezo huo baada ya Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ kuambaa na mpira upande wa kushoto na kupiga krosi ya kimo cha mbuzi ambayo iliwapita walinzi wa Yanga akiwamo kipa Diarra lakini Mosses Phiri alichelewa kuuwahi mpira na kupishanana nao sentimita chache akiwa kwenye lango la Yanga.
Yanga walijibu shambulizi hilo dakika 10 baadaye lakini Mayele alishindwa kuitumia vizuri pasi ya Kisinda kuipatia Yanga bao.
Dakika ya 50, Okrah tena akiwa na mpira alipiga shuti ambalo lilipaa juu ya goli la Yanga ambapo dakika mbili baadaye Yanga walibu shambulizi hilo baada ya Mayele kuuwahi mpira wa juu aliopigiwa na Moloko lakini kichwa alichopiga kilipaa juu ya lango la Simba.
Okrah kwa mara nyingine dakika ya 68 aliambaa na mpira mbele ya mabeki wa Yanga ambao walikuwa kama wanamsindikiza lakini shuti lake la chinichini lilitoka kulia kwa Diarra ambaye alichukizwa na jambo hilo na kuwauata mabeki wake huku akiwalaumu hadi mwamuzi akamtaka arudi golini.
Katika mechi hiyo rafu za hapa na pale zilitawala huku mwamuzi Kayoko akitoa kadi za njano katika kukabiliana na matukio hayo.
Kwa matokeo hayo, Simba inaendelea kushikilia usukani wa ligi ikiwa na pointi 14 sawa na Yanga lakini timu hizo zinatofautiana kwa mabao ya kufungwa, wakati Simba imefungwa mabao matatu, Yanga imefungwa matano, zote hadi sasa zimecheza mechi sita na kufunga mabao 12.
Soka Yanga, Simba zagawana pointi kibabe
Yanga, Simba zagawana pointi kibabe
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
