London, England
Kurejea kwa mshambuliaji, Gabriel Jesus katika kikosi cha Arsenal kumemfurahisha kocha Mikel Arteta ambaye anamuona mchezaji huyo aliyekuwa majeruhi tangu Novemba kama usajili mpya.
Juzi Jumamosi, kwa mara ya kwanza tangu alipoumia wakati akiiwakilisha Brazil kwenye fainali za Kombe la Dunia, Gabriel Jesus alirejea katika kikosi cha kwanza Arsenal na kufunga mabao mawili katika ushindi wa 4-1 dhidi ya Leeds United.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Man City, alipata maumivu ya goti na Jumamosi aliichezea Arsenal kabla ya kutolewa katika kipindi cha pili ambapo mashabiki walimpa heshima wakati akitoka uwanjani.
Mabao mawili ya mchezaji huyo yamesaidia kuimarisha mbio za Arsenal katika kulisaka taji la Ligi Kuu England ikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo kwa tofauti ya pointi nane dhidi ya Man City inayoshika nafasi ya pili.
“Tumefurahishwa naye, wote wamefurahia, sote tulimpigia makofi, amekuwa akifanya juhudi kubwa katika miezi minne au mitano iliyopita akipewa msaada mkubwa kwenye timu na maofisa,” alisema Arteta.
“Leo (Jumamosi) amekuwa na haki ya kuwa kwenye kikosi cha kwanza, amepata nafasi akiwa mwenye shauku na akapata mabao mawili,” alisema Arteta.
Matokeo ya mechi za EPL mwishoni mwa wiki…
Man City 4-1 Liverpool
Arsenal 4-1 Leeds United
Bournemouth 2-1 Fulham
Brighton 3-3 Brentford
Crystal Palace 2-1 Leicester City
Nottingham Forest 1-1 Wolverhampton
Chelsea 0-2 Aston Villa
West Ham 1-0 Southampton
Newcastle 2-0 Man United