Doha, Qatar
Mshambuliaji wa Argentina, Lautaro Martinez amesema mechi yao ya leo Jumamosi na Mexico kwenye Kombe la Dunia ni kama fainali baada ya kupoteza mechi ya kwanza dhidi ya Saudi Arabia huku kocha wa Mexico, Gerardo ‘Tata’ Martino akisema atafanya kila liwezekanalo kuitoa Argentina.
Argentina, mabingwa mara mbili wa Dunia, ni moja ya timu zilizopewa nafasi ya kuwa na uwezo wa kubeba taji la dunia mwaka huu lakini ilianza mbio hizo kwa kuushangaza ulimwengu wa soka baada ya kupoteza mechi ya kwanza kwa kufungwa mabao 2-1 na Saudi Arabia.
Matokeo tofauti na ushindi katika mechi na Mexico yataiweka njia panda Argentina katika mbio za kuwania kufuzu hatua ya mtoano ikitokea Kundi C. “Ni mechi itakayoweka wazi hatma yetu kwenye Kombe la Dunia,” alisema Martinez.
Katika mechi na Saudi Arabia nahodha wa Argentina, Lionel Messi aliipatia timu hiyo bao kwa mkwaju wa penalti lakini Saudi Arabia walifanikiwa kusawazisha bao hilo na kuandika bao la pili ingawa mabao matatu ya Argentina yalikataliwa kwa madai wafungaji waliotea.
“Ni pigo kubwa kwa morali tuliyokuwa nayo, lakini hili ni kundi imara na ambalo liko pamoja, tunahitaji kutulia, kujiweka sawa na kufikiria yajayo, mechi inayokuja ni dhidi ya Mexico, kwa hiyo ni lazima fikra zetu ziwe katika kupata ushindi na si vinginevyo,” alisema Martinez.
“Tuna matarajio ya ushindi, na nafikiri tulishindwa (na Saudi Arabia) kwa sababu ya mambo madogo madogo, ni kutokana na makosa yetu, tumewasoma wapinzani wetu na nafikiri tupo tayari,” alisema Martinez.
Kocha wa Argentina, Lionel Scaloni alisema kwamba mchezaji wake, Messi yuko fiti licha ya kuwapo habari kwamba alikuwa na maumivu ya enka na kikosi chake kitajibu mapigo baada ya kupoteza mchezo wao wa kwanza.
Kwa upande wake kocha Martino wa Mexico ambaye ni mzaliwa wa Argentina, amesema kwamba atafanya kila liwezekanalo ili timu yake iweze kutoka uwanjani na ushindi mbele ya Argentina na staa wao Messi.
Martino aliyewahi kuwa kocha wa Messi katika klabu ya Barcelona msimu wa 2013-14 ameamua kuwa wazi kwenye mkutano na waandishi wa habari kuhusu nia yake ya kuhakikisha anaifunga Argentina baada ya sare ya 0-0 na Poland katika mechi yao ya kwanza.
“Ungefanya nini kama wewe ungekuwa kwenye nafasi yangu, najua nilizaliwa wapi, naweza kukutajia mwaka, hospitali niliyozaliwa, hata namba ya mji lakini bado nitafanya kila liwezekanalo kwa ajili ya Mexico kupata ushindi.
Mechi za leo Jumamosi…
Kundi C
Poland v Saudi Arabia, saa 10:00 alasiri
Argentina v Mexico, saa 4:00 usiku
Kundi D
Tunisia v Australia, saa 7:00 mchana
Ufaransa v Denmark, saa 1:00 usiku
