Belek, Uturuki
Timu ya soka ya taifa ya Iran imeingia uwanjani na vitambaa vya rangi nyeusi na mabegi ya watoto wa shule kabla ya mechi yao na Nigeria ikiwa ni ishara ya kupinga mashambulizi yaliyosababisha maafa katika moja ya shule nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa za nchini Iran, vita inayoendelea kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran katika siku yake ya kwanza ilisababisha vifo vya watu wapatao 168 wakiwamo watoto 110 waliokuwa shule.
Mashambulizi hayo ya anga yalifanywa katika Shule ya Shajareh Tayyebeh Kusini mwa Iran ingawa taarifa za nchini Marekani zinadai kuwa mashambulizi hayo yalifanywa kimakosa na jeshi la nchi hiyo.
Katika kupinga mashambulizi hayo, kabla ya kuanza kwa mechi ya kirafiki na Nigeria mjini Balek, Uturuki, wachezaji wa Iran walionekana wakiwa na mabegi ya watoto wakiongozwa na mshambuliaji nyota wa zamani wa klabu za FC Porto na Inter Milan, Mehdi Taremi.
Taarifa ya chanzo kimoja nchini Iran ilieleza kuwa wachezaji hao wamebeba mageni ya rangi ya pinki na zambarau ili kuwakumbuka watoto wa shule waliouliwa katika shambulizi lililofanywa na Jeshi la Marekani.
Maofisa wa Iran walizilaumu Marekani na Israel kwa shambulizi walilofanya kwenye shule hiyo ambayo ipo karibu na kituo kimoja cha jeshi ingawa nchi hizo mbili hazijakiri kuhusika na shambulizi hilo.
Iran ni kati ya nchi ambazo zimefuzu kushiriki fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico ingawa ushiriki wa Iran upo njia panda kwa kuwa haitaki mechi zao zichezwe Marekani licha ya ratiba kupangwa hivyo.
Fainali za Kombe la Dunia zimepangwa kuanza Juni 11, 2026 na Iran imechukua msimamo wa kukataa kupeleka timu Marekani hasa baada ya rais wa nchi hiyo, Donald Trump kusema kuwa anawakaribisha Iran lakini hawezi kuwahakikishia usalama wao.
Wakati huo huo, Iran imepiga marufuku timu zao za michezo kwenda katika nchi ambazo zina ugomvi nao, kauli ambayo imekuja wakati timu ya soka ya Traktor Sazi ya nchini Iran ikijiandaa kwenda Saudi Arabia.
Traktor ikiwa Saudi Arabia inatarajia kucheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Asia dhidi ya Shabab Al Ahli ya Dubai, mechi iliyopangwa kuchezwa Alhamisi ijayo.
Taarifa ya katazo hilo imetolewa na Wizara ya Michezo ya Iran na huenda ikaathiri moja kwa moja ushiriki wa Iran kwenye Kombe la Dunia kama Fifa hawatohamisha mechi za taifa hilo na kuzipeleka katika nchi nyingine mwenyeji kati ya Mexico au Canada.
Kimataifa Wachezaji Iran wabeba mabegi ya shule kuipinga Marekani
Wachezaji Iran wabeba mabegi ya shule kuipinga Marekani
Read also
