Na mwandishi wetu
Katibu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha amewataka makocha, mapromota, waamuzi na mabondia walioshiriki mafunzo yaliyoandaliwa na Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) kuyatumia mafunzo hayo kuleta mabadiliko kwenye mchezo wa ngumi nchini.
Semina ya mafunzo ya siku tano iliyoandaliwa na TPBRC inafanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam tangu juzi ikitarajiwa kumalizika Novemba 20, mwaka huu.
Akizungumza leo, Msitha amewataka makocha, mapromota na waamuzi kuachana na desturi ya Watanzania kupata elimu na kushindwa kuifanyia kazi na badala yake wabadilike kwani watapata fursa nyingi wakiyatumia mafunzo hayo kwa vitendo.
“Mchezo wa ngumi kwa Tanzania unashika nafasi ya pili baada ya soka, kwa sababu mchezo huu wa masumbwi kwa sasa umekuwa kipaumbele kikubwa, kwa hali hiyo waamuzi wanapaswa kufanya vizuri kuepuka na kashfa na kufanya kazi kwa weledi ili kuvutia wadhamini kuleta fedha nyingi.
“Shughuli za michezo zinahitaji utayari na mapenzi kutoka moyoni, niwapongeze kwa wale wote walijitokeza katika kupata elimu hii,” alisema Neema.
Kwa upande wake Katibu wa TPBRC, Yahya Poli alisema, ”mafunzo haya siyo mara ya kwanza ila ukubwa huu ni mara ya kwanza kwa sababu wamekuja washiriki kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania wakiwemo mapromota, madaktari, makocha na waamuzi kuja kupata mafunzo haya ya siku tano, hivyo ni vizuri kwa tasnia.”
Ngumi Msitha ataka mafunzo ya ngumi yatumike
Msitha ataka mafunzo ya ngumi yatumike
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
