Na Hassan Kingu
Uamuzi wa kumuondoa kocha Kim Poulsen kuinoa Taifa Stars unapata uhalali kwa kuzingatia matokeo ya hivi karibuni ya timu hiyo lakini uamuzi huo hauwezi kuwa suluhisho la matokeo mabaya ya Stars.
Stars ambayo hivi karibuni tumeishuhudia ikipata tabu kupata matokeo dhidi ya Somalia tena katika mechi mbili za kwenye uwanja wa nyumbani, iliwashangaza wengi na katika hali ya kawaida ilianza kuibua uwezekano wa kuchukua maamuzi magumu.
Hatimaye maamuzi magumu yakaanzia kwa kocha Poulsen kutoka Denmark ambaye amekabidhiwa majukumu ya timu za vijana, ni kazi ambayo inaaminika kwamba anaimudu vyema kwani amewahi kuifanya mwaka 2011 na 2012 na wadau wengi wa soka wakaonekana kuifurahia kazi yake kabla ya kuwa kocha mkuu kuanzia 2012 hadi 2014.
Tangu wakati huo, Poulsen ameingia na kutoka Tanzania mara mbili kwa hiyo si mtu mgeni na soka la Tanzani na ni dhahiri kwamba anajua mengi mazuri na mabaya ya soka la Tanzania, anajua nini kinalikwaza soka la Tanzania na nini kinaweza kufanywa ili kujikwamua.
Kilichomkuta Poulsen naamini tupo baadhi yetu, tena wengi tu ambao tulikitarajia, matokeo mabaya, achana na haya ya Uganda Cranes ya kufungwa bao 1-0, matokeo dhidi ya Somalia yalituumiza na kutufanya tusubiri nini kitawakuta waheshimiwa wa kwenye benchi la ufundi, hatimaye Poulsen na wenzake wakafanywa wahanga.
Uamuzi wa kumuondoa Poulsen hata hivyo tusijidanganye kwamba unaweza kutusaidia kwa namna yoyote kuifunga Uganda Cranes kwao, na japo dakika 90 zinaweza kuwa na maajabu yake lakini si kweli kwamba Poulsen na wenzake ndio waliokuwa kikwazo.
Tunachokiona kwenye timu za Yanga, Simba, Azam, Singida Big Stars na timu nyinginezo ni kielelezo cha timu yetu ya Taifa kuwa na wakati mgumu, kutokuwa na wachezaji wenye uwezo wa kuisaidia timu kupata mafanikio.
Ukikiangalia kikosi cha kwanza cha Yanga, Simba, Azam, Singida Big Stars unauona ukweli huo wachezaji tegemeo wengi wao ni wageni na kadri siku zinavyozidi kwenda jambo hili linazidi kuwa kubwa, hata wale wachezaji wageni wanaoachwa na Yanga, Simba na Azam baadaye wanarudi na kucheza katika timu nyingine.
Tumeliona hilo kwa Paschal Wawa, Meddie Kagere na wengineo na hali hiyo itaongezeka, maana yake ni kwamba hawa wageni wataendelea kutawala hata timu nyingine, Singida Big wameanza, itakuwa hivyo hivyo kwa Coastal Union, Mtibwa Sugar, Geita Gold, Namungo na nyinginezo na kimsingi hili ni jambo zuri kwani linatoa fursa ya kuwapo ushindani miongoni mwa wachezaji na hivyo kuchangia maendeleo ya soka.
Tumezoea kuona wachezaji wanaoachwa Simba, Yanga na Azam kujiunga na timu nyingine za Ligi Kuu ya NBC lakini sasa idadi imeongezeka, hizo timu za chini pia ni kimbilio kwa wachezaji wageni ambao wanapokosa soko Yanga, Simba na Azam, kimbilio linakuwa ni timu nyingine ya Ligi Kuu.
Nini maana yake?
Maana yake ni kwamba Ligi Kuu yetu inazidi kuwa maarufu na yenye nguvu ya kifedha ndio maana imekuwa rahisi kwa wachezaji kutoka nje kuzikimbilia timu ambazo pengine miaka ya nyuma wasingekuwa tayari kujiunga nazo lakini taratibu zimeanza kuwa kimbilio lao.
Nini matokeo ya hili?
Anachokutana nacho Poulsen katika timu ya Taifa kinaonekana pia katika jambo hili, uteuzi wa wachezaji unampa wakati mgumu, anaiangalia ligi inayoonekana kuwa na mvuto na ushindani lakini wachezaji mahiri na wenye uwezo wengi wao ni wageni.
Mfano huu ukiutaja wapo watu wanaoitaja Ligi Kuu England ambayo ni kweli imejaa wachezaji wageni lakini mfano huu hauna uhalisia unapoiangalia England na Tanzania.
Ukiitaja England unaitaja timu ambayo ikikosa kushiriki fainali za Kombe la Dunia dunia haikaliki, kelele kila kona, ni nchi ambayo inawaza kulibeba Kombe la Dunia, si kushiriki fainali za Kombe la Dunia, ni nchi inayohaha ni lini italibeba taji la Ulaya na si kushiriki fainali za Ulaya.
Kwa hiyo kuilinganisha England na Tanzania katika soka ni kutoitendea haki Tanzania. England ipo mbali sana na zaidi ya yote wachezaji wazawa wa England wanapigania namba katika klabu zao.
Nini kifanyike?
Kinachotakiwa kufanyika kwa sasa ni kwa wachezaji wazawa kutambua kwamba wapo kwenye ligi yenye ushindani na hivyo hawawezi kuukwepa ushindani eti kwa sababu tu wao ni wazawa, hilo halipo, ni lazima wapambane kupigania namba vinginevyo wajiandae kisaikolojia kuwa wachezaji wa kudumu wa akiba, na hili si kwenye Yanga, Simba na Azam tu bali hata timu nyingine kwani huko nako wageni wameanza kuwafuata kama ambavyo tumeona kwa Singida Big, Geita Gold na kwingineko.
Wachezaji wazawa ni lazima wafahamu kwamba timu wanazozichezea zinataka mafanikio, wafadhili hao tunaowasikia wakiwekeza mamilioni ya shilingi kwenye soka wanataka mafanikio ambayo yatawawezesha kupata faida itokanayo na biashara ya soka.
Hakuna tajiri anayewekeza mamilioni ya fedha zake bure kwenye soka au anatoa sadaka kwenye soka, hakuna kitu kama hicho bali wapo kwenye biashara ya soka wakitaka faida na wa kuwasaidia kupata mafanikio au faida kupitia soka ni wachezaji wazuri na wenye uwezo ambao tajiri akiwakosa Tanzania hatoona tabu kuwasaka nje ya nchi.
Tumeliona hilo kwa Aziz Ki jinsi Yanga walivyohaha kumpata na hata kuwa tayari kutoa fedha nyingi, ni kwa sababu wanataka awape mafanikio, tumeona mmiliki wa Azam akitoka hadharani na kusajili wachezaji na bila shaka tutaendelea kuyaona hayo kwa wengine.
Kwa wachezaji wazawa niwakumbushe tu kwamba wasipoangalia hata kwenye timu ya Taifa watakuwa ni wachezaji wa akiba na wakati mwingine hata fursa ya kuitwa kwenye timu hiyo wasiipate kwani tayari baadhi ya wageni wameanza kuiona fursa kwenye timu hiyo na wanaangalia mazingira ya kuwawezesha kupata uraia wa Tanzania, na niwakumbushe tu hili ni jambo la kawaida, limeshatokea nchi nyingi na pengine huu ni wakati wa wachezaji wazawa kujiandaa nalo.
Tuchukulie mfano mchezaji mzuri wa Jamhuri ya Kidemokrasia wa Kongo (DRC) ambaye hapati nafasi kwenye timu ya DRC akiiona fursa Tanzania labda ana ndugu wenye asili ya Tanzania au ana nasaba yoyote na Tanzania, hatoona tabu kuangalia uwezekano wa kubadili uraia, akiona kuna fura hiyo hatoona tabu kufanya hivyo hasa anapokuwa na uhakika timu hiyo inaweza kufuzu Afcon na yeye kupata fursa ya kujitangaza kwa kutumia mashindano hayo.
Kocha wa timu ya Taifa hawezi kumuacha mchezaji mzuri wa aina hii eti kwa sababu si Mtanzania wa kuzaliwa, na kama anamhitaji na mazingira ya kisheria hayambani anaweza hata kumshawishi mchezaji huyo abadili uraia ili tu amuite kwenye timu ya Taifa.
TFF ifanye nini?
Nadhani huu ni wakati kwa TFF kuliangalia jambo hili kwa mapana, ni vipi wachezaji watawekewa mazingira au watakuwa na utayari wa kwanza kutambua kwamba wapo kwenye ushindani na kujiandaa kukabiliana na ushindani kwani naona kama dhana nzima ya kupigania namba au kushindania namba hawana au hawaipi umuhimu, niliwahi kusikia habari ya mchezaji mmoja maarufu aliyepewa sifa zote lakini sasa anasugua benchi, mchezaji huyo huyo inadaiwa aliwahi kusema kwamba hana tatizo na benchi kwa kuwa anapata mshahara wake kama kawaida, mchezaji wa aina hii ni wazi kwamba dhana nzima ya kushindana haipo katika fikra zake kwani hata kitendo cha kuwekwa benchi hakimsumbui.
Kupambana kwao na kutambua kwamba wapo kwenye ushindani, si tu kutawasaidia wao kujihakikishia namba katika timu zao na kuneemeka na biashara ya soka inayoendelea kukua katika nchi yao bali pia kutakuwa na maana kubwa kwenye timu ya Taifa, tofauti na hivyo TFF itaendelea kulaumiwa kila siku na timu ya Taifa itaendelea kufanya vibaya na TFF itaendelea kujidanganya kwamba suluhisho ni kumuondoa kocha kama ilivyofanywa kwa Poulsen.
Kimataifa Je TFF iko sahihi kumuondoa Poulsen?
Je TFF iko sahihi kumuondoa Poulsen?
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
