Munich, Ujerumani
Rais wa klabu ya Bayern Munich, Herbert Hainer amemwambia rais wa Real Madrid, Florentino Pérez kuwa klabu yake haitosikiliza ofa ya kumuuza mchezaji wao nyota Michael Olise (24).
Perez ambaye hivi karibuni ameshinda uchaguzi wa nafasi ya urais wa Real Madrid, kabla ya uchaguzi huo alitangaza nia ya kuweka rekodi ya usajili kwa kutumia Pauni 150 milioni kusajili wachezaji wa hadhi ya juu maarufu Galactico.
Baada ya kuwapo habari kwamba Perez ana nia ya kumsajili Olise, Hainer alizungumza na jarida la Bild la nchini Ujerumani na kubainisha kuwa Olise ni mchezaji wa Bayern Munich na hawamuuzi.
“Michael Olise ni mchezaji wa Bayern Munich ambaye ana mkataba mrefu, na sisi si klabu inayouza wachezaji, kama Florentino Perez anataka kutuletea ofa, aihifadhi, hilo ni tatizo,” alisema Hainer.
Bayern ilimsajili Olise, Juni 2024 kutoka klabu ya Crystal Palace ya England na winga huyo kutoka Ufaransa alisaini mkataba na klabu hiyo unaofikia ukomo Juni 2029.
Akiwa na Bayern hadi sasa Olise ana mabao 15 na asisti 32 na timu yake imefanikiwa kulitetea vyema taji la Ligi Kuu Ujerumani maarufu Bundesliga msimu wa 2025-26 uliomalizika mwezi uliopita.
Olise pia alitangazwa kuwa mchezaji bora wa msimu katika Bundesliga na pia alitajwa katika timu ya msimu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kufunga mabao matano na kutoa asisti saba katika mechi 13.
Kwa sasa Olise yumo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa kwenye fainali za Kombe la Dunia wakisubiri kuingia dimbani dhidi ya Senegal, mechi itakayopigwa Jumanne, Juni 16, 2026.
