Hatimaye Argentina imebeba Kombe la Dunia baada ya miaka 36 ikiwabwaga mabingwa watetezi Ufaransa kwa mikwaju ya penalti 4-2, matokeo yaliyokuja baada ya dakika 120 za mpambano wa kukata na shoka ulioisha kwa sare ya mabao 3-3.
Ushindi huo pia unakuwa tukio kubwa kwa nahodha na mshambuliaji wa Argentina Lionel Messi ambaye sasa anaongeza medali nyingine kubwa iliyokosekana katika kabati lake lenye medali kibao alizobeba katika soka la hadhi ya juu.
Kylian Mbappe ndiye aliyekuwa kwa kwanza kupiga penalti ya Ufaransa na kuujaza mpira wavuni akifuatiwa na nyota mwenzake wa PSG, Messi ambaye naye alijibu mapigo kwa kuifungia bao Argentina.
Baada ya Gonzalo Montiel kupiga penalti ya mwisho na kuujaza mpira wavuni, Messi alikuwa wa kwanza kuanguka chini katikati ya uwanja kwa furaha kabla ya kuzungukwa na wachezaji wenzake wakishangilia taji ambalo mara ya mwisho Argentina ililibeba mwaka 1986 katika timu iiyokuwa chini ya nahodha, Diego Maradona.
Katika mikwaju ya penalti, shujaa mwingine wa Argentina alikuwa ni kipa wao, Emiliano Martinez ambaye pia anaidakia Aston Villa ya England kwa namna alivyookoa penalti ya Ufaransa hasa ile iliyopigwa na Kingsley Coman.
Awali ni Argentina waliibua matumaini makubwa ya kumaliza mchezo huo katika dakika 90 za kawaida baada ya kupata mabao mawili katika dakika za 23 na 36 yaliyofungwa na Messi kwa mkwaju wa penalti iliyotolewa baada ya Ausmane Dembele kumchezea rafu, Angel di Maria wakati akielekea kuonana na kipa Hugo Lloris wa Ufaransa.
Messi aliupiga mpira huo kwa ufundi akimchambua Lloris aliyeangukia upande wake wa kulia na mpira kwenda wavuni kupitia upande wake wa kushoto. Di Maria alifunga bao la pili kwa mpira ulioanzia kwa Messi aliyempasia Mac Allister aliyetoa pasi ya mwisho kwa mfungaji.
Ufaransa ilibadili matokeo dakika 10 za mwisho kwa mabao yaliyofungwa na Mbappe ambaye alifunga la kwanza katika dakika ya 80 kabla ya kumalizia la pili kwa mkwaju wa penalti dakika moja baadaye hali iliyovuruga shamrashamra zilizoanza kuonekana kwa mashabiki wa Argentina na kugeuka kuwa huzuni na mshangao kwa mashabiki hao wasiamini kilichotokea.
Matokeo hayo yalizifanya timu hizo kuingia katika dakika 30 za nyongeza ambazo kwa mara nyingine, Argentina ilizitumia vizuri kupata bao lililofungwa kwa penalti na Messi dakika ya 108 lakini Mbappe tena alivuruga sherehe za Argentina kwa kusawazisha kwa penalti dakika ya 118 na kumfanya mchezaji huyo awe amefunga mabao manne katika mechi hiyo, matatu yakiwa ya penalti.
Argentina hadi kubeba kombe ilizianza fainali vibaya kwa kufungwa mabao 2-1 na Saudi Arabia katika mechi ya makundi, tukio linalowakumbusha mashabiki kilichoikuta Hispania mwaka 2010 katika fainali za Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini, timu hiyo pia ilipoteza mechi yake ya kwanza ya makundi kwa kufungwa bao 1-0 na Switzerland lakini mwishowe kama Argentina nayo ikabeba taji.
Kimataifa Argentina yabeba Kombe la Dunia
Argentina yabeba Kombe la Dunia
Read also