Manchester, England
Marcus Rashford ameendelea kuwa moto, mabao mawili aliyofunga kati ya matatu katika ushindi wa Man United wa mabao 3-0 dhidi ya Leicester jana Jumapili umedhihirisha hilo.
Ni mabao ambayo si tu yameimarisha rekodi yake ya mabao bali pia yameimarisha mbio za Man United katika kujiimarisha kwenye Ligi Kuu England (EPL), katika mbio za top four au hata kubeba taji.
Man United inashika nafasi ya tatu EPL ikiwa na pointi 49, imezidiwa na vinara Arsenal kwa tofauti ya pointi tano na tatu kwa Man City wanaoshika nafasi ya pili, ni hatua nzuri katika kulisaka taji.
Kwa Rashford katika EPL amefikisha mabao 14 akiwa ameachwa mbali na Erling Haaland wa Man Ciy anayeongoza akiwa na mabao 26 na Harry Kane wa Spur anayeshika nafasi ya pili akiwa na mabao 17.
Rekodi ya Rashford hata hivyo inatoa picha ya kielelezo cha mafanikio ya mshambuliaji ambaye amedhihirisha ubora wake tangu kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia Desemba mwaka jana.
Tangu kumalizika kwa fainali hizo, Rashford amefunga mabao 17 katika mechi 18, rekodi ambayo ni nzuri kwa mshambuliaji yeyote wa kiwango cha juu.
Ubora wa Rashford ambaye kwa msimu huu amefikisha jumla ya mabao 24, ni kama vile umeshtuliwa na fainali za Kombe la Dunia, kabla ya hapo hakutisha, kulikuwa na hofu kwamba huenda angeachwa katika kikosi cha England.
Baada ya fainali hizo ni kama vile mshambuliaji huyo ameuwasha moto, kasi imeendelea na kwa sasa amekuwa akipambwa kila kona kutokana na kujiamini na umakini wa hali ya juu anapolikaribia lango.
Amedhihirisha hayo kwa vitendo, sifa hizo ndizo zilizomfanya kocha wa Barca, Xavi Hernandez kumtaja kuwa mshambuliaji hatari kabla ya mechi ya Europa Ligi baina ya timu hizo iliyoisha kwa sare.
Pengine ni sifa hizo hizo ndizo ambazo zimewafanya matajiri wa klabu ya PSG ya Ufaransa kutangaza kwamba Rashford ni mmoja wa wachezaji ambaye wangependa kumsajili katika timu hiyo ya Paris.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25 sasa atakuwa amebakisha mambo mawili kabla ya kumalizika kwa msimu, moja ni kubeba taji la EPL akiwa na Man United na pili ni kuibuka mfungaji bora.
Kubeba taji la EPL vita yake imefika patamu, timu hiyo kushika nafasi ya tatu si jambo dogo, ni ishara njema na hatua nzuri katka mbio hizo lakini kwenye kiatu cha mfungaji bora kazi bado nzito, anahitaji mabao 12 ili kumpiku Haaland, si kazi ndogo japo inawezekana.
Matokeo ya mechi za EPL wikiendi hii
Man United 3-0 Leicester City
Tottenham 2-0 West Ham
Aston Villa 2-4 Arsenal
Brentford 1-1 Crystal Palace
Brighton 0-1 Fulham
Chelsea 0-1 Southampton
Everton 1-0 Leeds United
Nottingham 1-1 Man City
Wolverhampton 0-1 Bournemouth
Newcastle 0-2 Liverpool
Kimataifa Rashford azidi kuwa moto EPL
Rashford azidi kuwa moto EPL
Read also