Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa Tanzania anayecheza soka la kulipwa timu ya Al Nassr ya wanawake ya Saudi Arabia, Clara Luvanga, ameendelea kung’ara katika Ligi Kuu Saudi Arabia akiwa kinara wa mabao kwenye ligi hiyo.
Clara amekuwa na muendelezo mzuri tangu alipotua Al Nassr akitokea Ludogrono ya nchini Hispania hadi sasa akiwa amepachika mabao sita katika michezo mitano aliyoshuka dimbani.
Katika orodha hiyo ya vinara wa mabao, Clara anafuatiwa kwa karibu na Mtanzania mwenzake, Enekia Kasonga anayekipiga Eastern Flames akiwa na mabao matano kibindoni.
Akizungumza leo Jumapili juu ya mafanikio yake hayo, Clara alisema kwamba anafurahia kiwango chake hivi sasa kwani malengo yake ni kucheza kwenye ligi bora zaidi ya aliyopo hivi sasa.
“Nafurahi kuwa hapa, mazingira yake pamoja na sapoti ninayoipata kwa wachezaji wenzangu na benchi la ufundi inanifanya nizidi kuimarika zaidi na kufanya vizuri kwenye michezo ninayopata nafasi,” alisema Clara.
“Malengo yangu ni kuisaidia timu yangu kushinda ubingwa lakini pia mimi binafsi nahitaji kushinda kiatu cha ufungaji bora kama nitamaliza msimu salama bila kupata majeraha,” alisema Clara nyota wa zamani wa Yanga Princess.