Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa timu ya Tanzania, ‘Taifa Stars’, Adel Amrouche, amesema baada ya kupata pointi tatu ugenini kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Niger, akili na nguvu wamehamishia kwenye mchezo ujao dhidi ya Morocco.
Ushindi huo umeifanya Stars kushika nafasi ya pili kwenye kundi E ikiwa na pointi tatu sawa na Zambia lakini wakizidiwa kwa wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Stars itashuka dimbani keshokutwa Jumanne kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kuikabili Morocco kuwania tiketi ya kufuzu michuano ya Kombe la Dunia 2026 itakayofanyika katika nchi za Canada, Mexico na Marekani.
Mara ya mwisho Taifa Stars na Morocco kukutana katika kusaka nafasi ya kufuzu Kombe la Dunia ilikuwa Machi 24, 2013 na Tanzania kupata ushindi mnono wa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Mkapa, nahodha Mbwana Samatta akipachika mabao mawili na Thomas Ulimwengu bao moja.
Akizungumza baada ya mchezo na Niger jana Jumamosi, Amrouche alisema anaamini mechi na Morocco haitakuwa rahisi licha ya kuwa watakuwa nyumbani kwani wanakutana na timu bora barani Afrika.
“Tunapaswa kusahau matokeo ya mchezo uliopita tuangazie zaidi mechi iliyo mbele yetu ambayo ndio kipaumbele chetu na muhimu kwenye safari yetu ya kutafuta nafasi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026,” alisema Amrouche.
Nahodha wa Stars, Samatta, alisema ni pointi tatu muhimu kwa timu, ambazo zimepatikana baada ya wachezaji kupambana na kufanikisha ushindi huo na sasa nguvu wanahamishia kwenye mchezo ujao dhidi ya Morocco.
“Ni pointi tatu muhimu ugenini, vijana wamefanya kazi kuhakikisha hili linafanikiwa najisikia fahari kwa wote pamoja na pasi ya bao niliyoitoa.Tunarudi nyumbani kupambana tena haina kufeli,” alisema Samatta.
Naye Kiungo mshambuliaji wa Taifa Stars, Charles Mmombwa mfungaji wa bao pekee la Stars, anayecheza kwenye klabu ya Macarthur FC ya Ligi Kuu Australia alisema amefurahi sana kufunga bao la kwanza akiwa na timu ya taifa na anawashukuru Watanzania kwa sapoti yao.
“Nina furaha sana, asante Watanzania kwa sapoti yenu tunawashukuru sana bila nyie haikuwa rahisi kushinda mchezo huu muhimu,” alisema Mmombwa.