Barcelona, Hispania
Kocha wa Barca, Xavi Hernandez amemfariji mchezaji wa timu ya taifa ya Hispania, Jenni Hermoso aliyepigwa busu mdomoni na rais wa Shirikisho la Soka Hispania (REEF) aliyesimamishwa, Luis Rubiales.
Xavi pia amemshutumu Rubiales kwa kitendo hicho ambacho kimemuweka katika wakati mgumu kiongozi huyo na kujikuta akishutumiwa kila kona duniani akitakiwa ajiuzulu katika nafasi yake REEF.
Akiwa katika mkutano na waandishi wa habari hivi karibuni, Xavi alieleza kuchukizwa kwake na kitendo alichofanya Rubiales na kusisitiza kwamba yuko pamoja na Jenni katika kadhia iliyomkuta.
“Nataka niwatangazie kwamba ninatoa ushirikiano usio na mipaka kwa Jennifer Hermoso na wachezaji wengine,” alisema Xavi kabla ya kuanza mkutano na waandishi wa habari.
“Namlaumu rais wa Shirikisho la Soka Hispania kwa tabia aliyoionesha na nasikitika kwamba kwa sasa watu hawazungumzii tena mafanikio ya kihistoria ya timu kubeba Kombe la Dunia,” alisema Xavi.
Agosti 20 mwaka huu, Rubiales alimpiga Jenni busu ‘zito’ la mdomoni wakati wa shamrashamra za kufurahia ushindi wa timu ya wanawake ya Hispania iliyobeba Kombe la Dunia la Wanawake (WWC) baada ya kuilaza England bao 1-0.
Baadaye, Jenni, 33, alisema kwamba kitendo alichofanyiwa na Rubiales hakikubaliki na hakukuwa na makubaliano baina yao ingawa awali alinukuliwa akimtetea kiongozi huyo akisema kwamba furaha iliyopitiliza ndiyo iliyomfanya ampige busu la mdomoni.
Fifa imemsimamisha Rubiales kwa siku 90 kujihusisha na masuala ya soka na imeanza uchunguzi wa tukio hilo huku kiongozi huyo akitakiwa na makundi mbalimbali ajiuzulu ingawa mwenyewe amesema hayuko tayari kufanya hivyo.
Wakati huo huo mama mzazi wa Rubiales, Angeles Bejar ambaye alianza mgomo wa kula, ametoka hospitali alipolazwa baada ya hali yake kuwa mbaya kutokana na mgomo huo wa kushinikiza mwanaye asibughudhiwe kwa alichokifanya kwa kuwa kulikuwa na makubaliano.