Na mwandishi wetu
Kocha Msaidizi wa Simba, Juma Mgunda amewaomba mashabiki wao kuwa na subira na kuendelea kuipa sapoti timu yao katika mechi tatu zilizosalia kwenye Ligi Kuu NBC badala ya kuwazomea.
Kikosi cha Simba juzi kilifungwa na Azam FC mabao 2-1 na kutolewa kwenye michuano ya Kombe la FA (ASFC), huku pia ikiwa na nafasi finyu ya kutwaa ubingwa wa ligi kutokana na watani zao Yanga kuhitaji pointi tatu pekee ili kutawazwa mabingwa wapya msimu huu 2022-23.
Kocha huyo amekiri kuwa msimu huu umekuwa mbaya kwao kutokana na mwisho mbaya katika mashindano yote waliyokuwa wakishiriki lakini hilo halipaswi kuwa kigezo cha mashabiki wao kuwazomea.
“Wote hatukufurahishwa na kilichotokea sababu malengo yetu yalikuwa ni kufanya vizuri kwenye mashindano yote, bahati mbaya malengo hayajatimia, inauma lakini kwenye mpira haya yanatokea naamini tutajipanga vizuri na msimu ujao tutarudi tukiwa imara zaidi,” alisema Mgunda.
Mgunda amesema kuwazomea wachezaji na benchi la ufundi hakuwezi kubadili yaliyotokea, cha msingi ni vyema mashabiki wao wakaendelea kuipa sapoti timu yao ili ifanye vizuri kwenye mechi zilizobaki ambazo ni muhimu pia kwao.