Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa Yanga, Crispine Ngushi amejiunga na timu ya Coastal Union ya Tanga kwa mkopo wa miezi sita hadi mwisho wa msimu wa huu.
Ngushi ambaye alijiunga na Yanga msimu wa 2021/22 kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea Mbeya Kwanza alikokuwa kinara wa mabao lakini alishindwa kung’ara Jangwani kutokana na kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara.
Akizungumza leo Jumapili Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe alisema wamempeleka Ngushi kwenye kikosi cha Coastal Union ili apate muda wa kucheza na kuimarisha kiwango chake.
“Ngushi ni mchezaji mzuri ambaye amekuwa hapati muda wa kutosha wa kucheza kwenye kikosi cha Yanga hivyo tumeona tumpeleke Coastal Union ambako tunaamini kwa uwezo wake atapata muda wa kutosha wa kucheza ili kurejesha ubora wake.
“Bado tunamuhitaji Ngushi ndio maana tumemtoa kwa mkopo wa miezi sita ili aendelee alipoishia kwenye mashindano ya Mapinduzi ambako alikuwa na kiwango kizuri na kuonyesha mwanga wa kurejea kwenye ubora wake,” alisema Kamwe.