Na mwandishi wetu
Mwamba wa Lusaka, Clatous Chota Chama amekerwa na matokeo ya sare ya mabao 2-2 ambayo Simba iliyapata mbele ya Power Dynamos ya Zambia licha ya yeye kucheza vizuri na kufunga mabao yote ya timu yake.
Chama ambaye kwa mara nyingine alionesha uwezo binafsi katika mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyopigwa nchini Zambia, Jumamosi iliyopita, alisema kwamba hayo hayakuwa matokeo waliyoyataka.
Mchezaji huyo hata hivyo aliwatoa hofu mashabiki wa Simba akiwaambia kwamba wanajiandaa kujibu mapigo wakiwa nyumbani katika mechi ya marudiano.
“Huu si mwanzo tulioutaka lakini tutafanya vizuri nyumbani ambapo hakuna anayekuja na kuacha kupewa kichapo,” ilisomeka kauli ya mchezaji huyo kupitia mitandao ya kijamii.
Mbali na Chama mchezaji mwingine wa Simba aliyeumizwa na matokeo hayo ni kipa wa timu hiyo, Ayoub Lankerd ambaye aliwaomba radhi mashabiki kwa kuruhusu mabao mawili kwenye lango lake.
Kipa huyo ambaye hiyo ilikuwa mechi yake ya kwanza kubwa na Simba naye alinukuliwa kupitia mitandao ya kijamii akisema, “samahani mashabiki Simba, sikuwa vizuri kwenye ile mechi, niliruhusu mabao mawili lakini naahidi mechi ijayo nitakuwa bora.”
Kipa huyo alionekana kuwakera mno mashabiki wa Simba hasa kwa namna ambavyo aliruhusu bao la pili lililofungwa na kwa shuti la mbali la chinichini ambalo ilionekana mapema angeweza kulidaka lakini alikosa umakini.
Simba sasa inasubiri kurudiana na vinara hao wa Zambia katika mechi ya marudiano ambayo itapigwa jijini Dar es Salaam ambapo timu hiyo itakuwa ikiwania kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo.