Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Polisi Tanzania, Mwinyi Zahera amesema hesabu zake kwa sasa anawaza namna ya kumaliza ligi katika nafasi tano za juu na siyo kuiokoa timu kushuka daraja.
Timu hiyo inashika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa ligi ikiwa imekusanya pointi 14 katika michezo 20 ambayo imecheza hadi sasa.
Zahera ameelea kuwa usajili walioufanya kwenye dirisha dogo unampa jeuri ya kushinda mechi zilizosalia na kupanda hadi nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC iliyobakisha takriban mechi 10 kabla ya kufungwa rasmi pazia la msimu wa 2022-23.
“Najua watu wengi hawaamini lakini ukweli ni kwamba Polisi haitoshuka daraja, sababu tumesajili vizuri na tayari matokeo ya usajili wetu yameanza kuonekana katika mchezo uliopita ambao tuliifunga Namungo FC kwao Lindi,” alisema Zahera.
Kocha huyo aliyewahi kupita timu kadhaa nchini ikiwemo mabingwa watetezi Yanga, ameeleza kuwa anachojivunia katika usajili huo ni wachezaji wapya kuelewana kwa haraka na wachezaji waliokuwepo tangu mwanzo wa msimu na kushika haraka mifumo.
Alisema kwa namna alivyoijenga timu hiyo ana uhakika wa kushinda mechi sehemu yoyote ikiwemo viwanja vya ugenini ambavyo kwa kiasi fulani vimekuwa vigumu kupata ushindi.
Zahera amewataka viongozi wa timu hiyo kuondoa presha kwani timu yao kwa sasa ipo katika mikono salama na itaendelea kutamba kwenye ligi hiyo kwa misimu kadhaa ijayo.
