Na mwandishi wetu
Timu ya soka ya Taifa ya wasichana chini ya miaka 17, Serengeti Girls leo itakuwa na kazi nzito kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar dhidi ya Cameroon katika mechi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia.
Pamoja na uzito unaoweza kuhusishwa na mechi hiyo lakini ni kama vile mechi ya kumalizia kazi kwani timu hiyo inahitaji ushindi wowote au sare ili kufuzu fainali hizo zitakazofanyikia nchini India kati ya Oktoba 11 hadi 30 mwaka huu.
Na iwapo wadada hao watafungwa basi si chini ya mabao 4-0 hiyo ni baada ya kupata ushindi wa mabao 4-1 katika mchezo wa awali uliopigwa wiki mbili zilizopita ambao Serengeti ilikuwa ugenini mjini Yaounde Cameroon.
Kocha wa timu hiyo, Bakari Shime pamoja na kutambua faida ya ushindi mnono walioupata katika mechi yao ya awali, alisema kwamba mchezo huo utakuwa mgumu ingawa wamejiandaa kuhakikisha wanafanya vizuri na hatimaye kufuzu.
“Mchezo utakuwa mgumu maana kama tuliweza kuwafunga kwao hata wao wanaweza kufanya lolote ila tumejiandaa kuhakikisha tunashinda,” alisema Shime.
Akiizungumzia mechi hiyo itakayopigwa leo saa 10 alasiri, nahodha wa timu hiyo, Noela Luala ameahidi kufanya vizuri katika mchezo huo ili kumpa zawadi Rais Samia Suluhu Hassan kama alivyo Rais wa kwanza mwanamke na wao wawe timu ya kwanza ya wanawake kufuzu.
Serengeti Girls wameshacheza mechi tano katika mashindano haya na kushinda michezo minne kwa idadi kubwa ya mabao na kupoteza mmoja.
Katika mashindano hayo yatakayoshirikisha timu 16 duniani kote, kwa Afrika timu za Nigeria na Morocco zimeshafuzu baada ya kushinda michezo yao ya marudiano iliyochezwa jana huku ikisubiriwa timu nyingine ambayo itapatikana leo katika mechi ya Serengeti Girls na Cameroon.
Na ingawa katika soka lolote linaweza kutokea lakini bado Serengeti Girls inapewa nafasi kubwa ya kufuzu ikiwa na faida ya ushindi wa mabao 4-1 katika mechi ya awali na leo inanufaika kwa kuwa mwenyeji katika mechi hiyo ya marudiano.
Ukiacha michuano ya soka ya walemavu, Serengeti Girls iwapo itafuzu, itaweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya soka kufuzu michuano ya Kombe la Dunia.
