Na Hassan Kingu
Msimu wa soka 2022-23 umemalizika rasmi Jumatatu iliyopita, ukihitimishwa kwa mechi ya fainali ya Kombe la FA (ASFC) kwa Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam FC.
Huo ni ubingwa wa tatu kwa Yanga msimu huu baada ya awali kutwaa ndoo ya Ligi Kuu NBC zikiwa zimesalia mechi mbili kumalizika ligi lakini pia ikiwa imeshaweka kibindoni Ngao ya Jamii walioipata kwa kuifumua Simba mabao 2-1 katika mechi ya kuukaribisha msimu huu.
Yanga imekuwa na mafanikio makubwa msimu huu kwa kuweka alama nyingi sehemu mbalimbali walizotia mguu, ikiwemo kuweka rekodi kwa kuingia fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza.
Kwa Tanzania imekuwa mara ya pili baada ya kupita miaka 30 tangu Simba ilipofanya hivyo mwaka 1993 na kupoteza mbele ya Stella Abidjan ya Ivory Coast kwa kufungwa mabao 2-0.
Yanga yenyewe iliupoteza ubingwa huo baada ya kufungwa mabao 2-1 na USM Alger nyumbani kabla ya ushindi wa bao 1-0 ugenini lakini USMA ilitawazwa bingwa wa kombe hilo kwa mara ya kwanza kupitia kanuni ya bao la ugenini.
Mbali na hilo, msimu huu pia Yanga imeionesha Afrika makucha yake kwa kutoa mfungaji bora mwenye mabao mengi katika Kombe la Shirikisho, Fiston Mayele aliyefunga mabao saba, pia kwenye fainali ya michuano hiyo ikatoa kipa bora, Djigui Diarra ambaye alikuwa nyota wa mchezo.
Tanzania ya tano Afrika
Ukiachana na alama za Yanga, ni msimu huu pia ambapo Shirikisho la Kimataifa la Historia na Takwimu za Soka Duniani (IFFHS) likaitangaza Ligi Kuu ya Tanzania Bara kushika namba tano kwa ubora Afrika na 39 duniani.
Ligi namba moja ni Misri ikifuatiwa na Algeria, Morocco, Sudan wakati kidunia Brazil imeendelea kuwa ya kwanza na England ya pili. Tanzania imeweka rekodi ikitoka nafasi ya 62 kwa mwaka 2021 hadi nafasi ya 39 wakati IFFHS ikitangaza takwimu hizo mpya Januari, mwaka huu.
Hat-trick nyingi
Msimu huu ni miongoni mwa misimu ambayo imeshuhudiwa rekodi ya ‘hat-trick’ nane zikifungwa na wachezaji tofauti. Wachezaji wa Simba, John Bocco na Saido Ntibazonkiza kila mmoja amefunga ‘hat-trick’ mbili.
Wengine ni Ibrahim Mkoko wa Namungo, Jean Baleke (Simba) na Mayele na Stephane Aziz Ki wa Yanga ambao kila mmoja amefunga hat-trick moja.
Saido achangamsha ligi mwishoni
Kama inavyofahamika baada ya Yanga kutangaza ubingwa mapema, kilichobaki ilikuwa ni kuhitimisha msimu kwa mechi zilizosalia na kusubiri timu zitakazoshuka daraja lakini Saido akaibua upinzani mzito wa kuwania ufungaji bora zikiwa zimesalia mechi mbili kufungwa rasmi pazia la ligi.
Saido akiwa na mabao 10 nyuma ya Mayele aliyekuwa amefunga mara 16, akafunga mabao matano katika ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya Polisi Tanzania na kufikisha mabao 15 na kuibua hisia za ushindani huo mpya kwa wadau na wapenzi wa soka nchini.
Kasi yake hiyo ikawafanya watu waifuatilie tena kwa karibu ligi ikiwa mwishoni ili kubaini nani ataibuka kinara wa mabao hasa ukizingatia uhasimu wa timu za nyota hao.
Hata hivyo, katika mechi za mwisho, Saido alifunga mabao mawili na Mayele akafunga bao moja na wote kulingana kwa mabao 17, hivyo wote wakapewa kiatu cha ufungaji bora kama ilivyokuwa miaka sita iliyopita kwa Simon Msuva (Yanga) na Abdulrahman Mussa (Ruvu) wote kupewa viatu kwa kufunga mabao 14.
Fei Toto aitingisha nchi
Kingine kitakachobaki kwenye kumbukumbu ya wengi ni kuvurugana kwa Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Yanga akidai amevunja mkataba na timu hiyo na yuko huru.
Jambo ambalo halikuwaingia Yanga akilini, wakamburuza mchezaji huyo kwenye kamati za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kuamuliwa mchezaji huyo kurejea Yanga, lakini Fei naye hakukubaliana na hilo na kuendelea kuvutana.
Suala hilo limechukua miezi sita kabla ya wiki mbili zilizopita Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuingilia kati na kuwaomba Yanga kumalizana na kijana huyo na siku tatu baadaye, Azam FC ilitangaza kumsajili Fei kutoka Yanga baada ya pande hizo tatu kumalizana.
Manzoki kuibukia uchaguzi Simba
Kitendo cha Simba pia kumshusha mshambuliaji hatari wa Dalian Pro ya Ligi Kuu ya China, Cesar Manzoki raia wa DR Congo kwenye uchaguzi wao mkuu uliofanyika Januari mwaka huu kiliibua hisia mbalimbali.
Baadhi ya mashabiki na wanachama wa Simba walilipuka kwa hisia tofauti wakidai wanafanyiwa ‘utoto’ kuletewa mshambuliaji huyo wakati dirisha la usajili limefungwa na kuonekana kama alitumika kwenye kampeni za baadhi ya washiriki wa uchaguzi huo.
Wengine walifurahia ujio wake hasa baada ya nyota huyo kueleza kuwa timu anayoweza kuja kuitumikia ni Simba pekee na si wapinzani wa Wekundu hao, Yanga.
Kwa upande wa pili yaani Yanga, kauli hiyo hawakupendezwa nayo na kumfanya Manzoki kuzizima kwa wiki kadhaa nchini kupitia mijadala mbalimbali.
Sekeseke la SportPesa, Yanga
Mkataba wa Wadhamini Wakuu wa Yanga, SportPesa uliyumba baada ya timu hiyo kutangaza wadhamini wao wapya, Haier kuelekea michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
SportPesa walieleza kulilia haki yao ya kukaa kifuani na kwamba hawakuridhia wadhamini wapya kukaa kwenye nafasi yao hata kama kanuni za Kombe la Shirikisho Afrika ilieleza wazi kutotumika kwa nembo za wadhamini wa Kampuni za Michezo ya Kubashiri kwa timu shiriki.
Baada ya vuta nikuvute ya hapa na pale, mwisho walilimaliza suala hilo na kuendelea na safari yao ya pamoja licha ya kuwa tayari lilishaanza kuibua mihemko baina ya mashabiki wa Yanga na viongozi wa SportPesa.
Singida inabadilika kila wakati
Timu ya Singida Big Stars imekuwa na historia yake msimu huu. Kwanza imepanda daraja ikiwa na nyota wengi wanaohofiwa ligi kuu na kuonesha makali yake wakiwa na kocha mkongwe, Hans van Der Pluijm.
Licha ya ugeni wao, walionesha umwamba wao na kufanikiwa kumaliza ligi nafasi ya nne na kukata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza msimu ujao. Pia ilitinga nusu fainali ya Kombe la FA kabla ya kufungwa bao 1-0 na Yanga.
Singida pia imeingia kwenye rekodi ya kubadilishwa majina matatu ndani ya msimu mmoja. Wakati inapanda kutoka Championship ilikuwa ikiitwa DTB kabla ya kuitwa Singida BS zilipoanza mechi za ligi kuu.
Na kama ulivyosikia na kuona, tayari Singida imebadilishwa tena siku chache baada ya kukamilika kwa ligi na sasa inaitwa Singida Fountain Gate FC baada ya timu hiyo kuuzwa kwa Taasisi ya Fountain Gate.
Hayo ni machache kati ya mengi yaliyojiri msimu huu ambayo hayatasahaulika ikiwemo rekodi mbovu ya Polisi Tanzania ya kushuka daraja na kufungwa jumla ya mabao 14 katika mechi zao mbili za mwisho. Simba iliifunga mabao 6-1 na Azam ikaibonda mabao 8-0.
Yote kwa yote ulikuwa msimu wenye msisimko mkubwa, rekodi nyingi na mengi ya kujivunia kama nchi na soka lake ingawa yapo yanayobaki kama funzo na mengine ya kuyaendeleza kwa ajili ya kuendelea kuing’arisha Tanzania misimu ijayo.