Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Polisi Tanzania, Mwinyi Zahera amesema mechi yao dhidi ya Mtibwa Sugar itakuwa kama fainali kwa kuwa ndio imebeba matumaini yao ya kubaki Ligi Kuu NBC.
Maafande hao watakuwa nyumbani Uwanja wa Ushirika, Moshi Mei 15, mwaka huu kucheza na Mtibwa mchezo ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkali kutokana na timu zote mbili kuwa katika nafasi mbaya kwenye msimamo wa ligi.
Zahera ameeleza kuwa ushindi walioupata kwenye mchezo uliopita dhidi ya Ihefu umeamsha ari ya kupambana kwenye kikosi chake hivyo anaamini kwa maandalizi waliyofanya hata mchezo ujao watachukua pointi tatu.
“Ni mchezo muhimu kwetu najua utakuwa mgumu lakini naamini tutapata ushindi ambao utasaidia kujiweka angalau kwenye ‘play off’ na siyo kushuka daraja moja kwa moja,” alisema Zahera.
Kocha huyo alisema kwa nama ushindani ulivyo kwa sasa uwezekano wa kujinasua moja kwa moja na janga la kushuka daraja ni mgumu kwa hiyo wanapambana kuangukia kwenye mechi za mtoano na baada ya hapo watajipanga kucheza mechi hizo za mtoano ili kusalia Ligi Kuu.
Polisi ambayo mechi iliyopita waliifunga Ihefu mabao 2-1, ipo nafasi ya 15 ikiwa na pointi 22 wakati Mtibwa ipo nafasi ya 12 na pointi 29 huku zikiwa zimesalia mechi tatu kumaliza msimu.