Na mwandishi wetu
Simba imemaliza kwa kishindo mechi yake ya mwisho ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Stade Malien ya Mali huku ikiaga mashindano hayo katika hatua ya makundi kwa msimu huu wa 2025-26.
Ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Jumamosi Februari 14, Simba iliandika bao hilo pekee mapema dakika ya tatu ya mchezo, bao lililofungwa na Anicet Oura.
Ushindi huo wa mechi ya Kundi D hata hivyo haukuwa na maana yoyote kwa Simba badala yake ni ushindi wa mechi ya kukamilisha ratiba ya michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika.
Huo ndio ushindi pekee wa Simba katika kundi hilo, katika mechi zake sita za makundi timu hiyo imepoteza tatu, sare mara mbili na kushinda mechi moja.
Simba imemaliza kundi lake ikiwa mkiani baada ya kukusanya pointi tano wakati Malien wao walishafuzu na ndio vinara wa kundi hilo baada ya kukusanya pointi 11 na wanaungana na Esperance ya Tunisia ambayo pia imefuzu.
Esperance imefuzu hatua ya robo fainali ikiwa na pointi tisa baada ya ushindi wa nyumbani wa mabao 2-0 katika mechi na Petro Atletico ya Angola, mechi ambayo pia imechezwa siku moja na mechi ya Simba na Malien.
Timu nyingine zilizofuzu robo fainali ni Al Hilal ya Sudan na Mamelodi ya Afrika Kusini kutoka Kundi C ambapo Al Hilal imemaliza kundi hilo ikiwa kinara baada ya kukusanya pointi 11.
Katika Kundi B, Al Ahly ya Misri tayari imeshafuzu ikiwa imekusanya pointi tisa huku hatma ya timu ya pili ikisubiri matokeo ya mechi za Jumapili Februari 15, 2026 ambapo Yanga ya Tanzania itacheza na JS Kabylie wakati Al Ahly itaumana na AS FAR Rabat ya Morocco.
Yanga hadi sasa ina pointi tano wakati FAR Rabat ina pointi nane na kwa upande wa Kabylie ina pointi tatu na itacheza mechi yake na Yanga kukamilisha ratiba kwani haina nafasi ya kusonga mbele.
Kimataifa Simba yaaga ligi ya mabingwa kwa ushindi
Simba yaaga ligi ya mabingwa kwa ushindi
Read also
