Na mwandishi wetu
Uongozi wa klabu ya Simba umelitaka jeshi la polisi nchini kuwachukulia hatua za kisheria waliohusika kumfanyia fujo mwenyekiti wa klabu hiyo, Murtaza Mangungu.
Mangungu alijikuta katika kadhia hiyo kutoka kwa watu wanaodhaniwa kuwa mashabiki wa soka ambao walimbughudhi na kumtolea lugha chafu baada ya mechi yao na Esperance ya Tunisia iliyoisha kwa sare ya mabao 2-2.
Matokeo ya mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa Jumapili Januari Mosi, 2026 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam yamewakera baadhi ya mashabiki ambao inaaminika waliamua kumalizia hasira zao kwa Mangungu.
Katika tukio hilo, Mangungu alijikuta akizongwa na kama si juhudi za maofisa usalama wa uwanjani hapo huenda hali ingeweza kuwa mbaya kwa kiongozi huyo kwa namna ambavyo idadi ya mashabiki ilikuwa kubwa.
Taarifa ya klabu ya Simba iliyotolewa na mwenyekiti wa bodi ya klabu hiyo, Crecentius Magori muda mfupi baada ya mechi hiyo, ilieleza kusikitishwa na tukio hilo na kulitaja kuwa si la kiungwana na halikubaliki.
Magori katika taarifa hiyo alisema kuwa sambamba na kutoa pole kwa Mangungu lakini pia alifafanua kuwa tukio hilo halitafumbiwa macho.
Alilitaka jeshi la polisi kuchukua hatua za kisheria kwa wote waliohusika au kula njama katika tukio hilo dhidi ya Mangungu na bodi ya klabu hiyo haitavumilia wala kubariki mtu yeyote atakayeharibu taswira ya klabu kwa namna yoyote.
Mashabiki wengi wanaoaminika kuwa wa Simba walikerwa na matokeo ya sare ya 2-2 ambayo yamezidi kufifisha kama si kufuta matumaini ya timu hiyo kucheza hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Soka Simba: Waliomfanyia fujo Mangungu waadhibiwe
Simba: Waliomfanyia fujo Mangungu waadhibiwe
Read also
