Manchester, England
Kocha wa Man United, Ruben Amorim ameonya kuwa mshambuliaji Marcus Rashford anaweza kuendelea kuwekwa kando hadi atakapoanza kufikia kiwango bora kinachotarajiwa katika timu hiyo.
Hatma ya Rashford ambaye pia anaichezea England imeendelea kuwa njia panda baada ya kuachwa kwenye kikosi cha kwanza katika mechi tatu za hivi karibuni dhidi ya Man City, Tottenham Hotspur na Bournemouth.
Amorim amefafanua kwamba kitendo cha kutompa nafasi Rashford sababu ni kiwango chake mazoezini ingawa mchezaji huyo amewahi kusema anataka kuondoka katika klabu hiyo jambo ambalo pia Amorim amesema hana tatizo nalo.
“Itakapofika wakati nikaona kwamba ni sahihi kubadili kitu nitafanya hivyo lakini kwa sasa nitaendelea kufikiria kilicho bora kwa ajili ya timu,” alisema Amorim.
Amorim alisema kwamba anazungumza na mchezaji huyo kila siku na si kuhusu mahojiano aliyoyafanya na kusema yuko tayari kuondoka bali ni kuhusu kiwango chake.
“Ni uamuzi wangu, anataka kucheza, anajaribu hapo kinachobaki ni uamuzi wangu, ni mimi kuamua, najaribu kufanya kitu katika namna yangu na hivyo ndivyo tu ninayofahamu kama nisipofanya hivyo nitakayeshindwa ni mimi ingawa sitokuwa peke yangu,” alisema Amorim.
Alipoulizwa kuhusu nini Rashford anachoweza kukifanya ili afikiriwe kurudi kwenye kikosi cha kwanza, Amorim alijibu kwa kifupi, ”awe katika ubora ambao anaweza kuwa.”
